Faith Kipyegon ateuliwa kuwania taji la mwanariadha bora duniani kwa wanawake mara ya tatu

Faith mwenye umri wa miaka 29,alitajwa kuwa mwanamke wa kwanza duniani kuvunja rekodi ya mbio za 1500 na 5000 kwa wakati mmoja mwaka huu.

Muhtasari

•Kipyegon ambaye alivunja rekodi tatu za dunia  na kushinda mataji mawili ya dunia mwaka wa 2023,anaongoza orodha ya watu kumi na mmoja ambao wameteuliwa kuwania tuzo hilo mwaka huu.

Faith Kipyegon
Faith Kipyegon
Image: HISANI

Mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za mita 1,500 na 5,000 Faith Kipyegon kwa mara ya tatu ameteuliwa kuwania Tuzo ya mwanariadha bora wa kike mwaka 2023.

Kipyegon ambaye alivunja rekodi tatu za dunia  na kushinda mataji mawili ya dunia mwaka wa 2023,anaongoza orodha ya watu kumi na mmoja ambao wameteuliwa kuwania tuzo hiyo mwaka huu.

Faith mwenye umri wa miaka 29,alitajwa kuwa mwanamke wa kwanza duniani kuvunja rekodi ya mbio za 1500 na 5000 kwa wakati mmoja mwaka huu.

Hivi majuzi alifunga msimu wake kwa ushindi wa medali ya shaba katika maili moja kwenye mashindano ya dunia ya mbio za barabara.

Katika mazungumzo yake ya moja kwa moja na runinga ya Citizen,Faith amesema kuwa ana imani ya kuibuka mshindi kwenye kinyanganyiro hicho kutokana na juhudi zake wakati wa mashindano ya mbio.

Mwanariadha huyo, amewataka mashabiki wake wote ambao hufuatilia mbio zake kumpigia kura ili kumwezesha kuibuka mshindi wa tuzo hilo akisema kwamba,tuzo hilo litaleta heshima si kwake tu bali kwa Taifa.

Mabingwa wengine walioteuliwa ni pamoja na;Femke Bol wa Uholanzi mshindi wa mbio za mita 400 kuruka viunzi,Mjamaika Shericka Jackson mshini wa mbio za mita 200, Haruka Kitaguchi wa Japani mshindi wa kurusha mkuki, Yaroslva Mahuchikh  wa Ukraine mshindi wa kuruka,Mhispania Maria Perez ambaye ni mshindi wa matembezi ya mbio,Yulimar Rojas Mvenezuela  mshindi wa kuruka mara tatu pia yuko kwenye orodha,pamoja na Winfred Yavi wa Bahrain ambaye ni mshindi wa mbio za mita 3000 kuruka viunzi.

Kipyegon ni mwanamke wa kwanza Mkenya kushinda tuzo hiyo  baada ya Muethiopia Almaz Ayana aliyeshinda mwaka wa 2016.

Upigaji kura utakamilika Octoba 28,kisha washindi wa fainali  wanawake na wanaume kwa pamoja kutangazwa Novemba 13

Watakaoshinda kwenye fainali watatajwa Desemba 11.