Tanzia huku mwanariadha wa Kenya akifa maji wakati akijaribu kuokoa mbwa nchini Mexico

Familia ya marehemu inaomba usaidizi wa kuleta mwili wake kutoka Mexico hadi nyumbani kwao Bomet kwa mazishi mwafaka.

Muhtasari

•Kibet alikufa maji kwenye bwawa kwa bahati mbaya alipokuwa akijaribu kumuokoa mbwa wa  mwajiri wake mnamo siku ya Jumanne wiki jana, Desemba 12, 2024.

•Mjane wa Ngetich, Bi Janeth Ngetich alisema kwamba ni maelezo machache tu kuhusu kifo chake ambayo yamefichuliwa kwao.

Marehemu Josphat Ngetich
Image: HISANI

Muungano wa wanariadha wa Kenya na nchi nzima inamuomboleza mwanariadha wa zamani, Josphat Kibet Ngetich aliyepoteza maisha yake akiwa nchini Mexico.

Ngetich ambaye katika miaka ya awali aliwakilisha Kenya katika mashindano ya kimataifa anaripotiwa kufa maji kwenye bwawa kwa bahati mbaya alipokuwa akijaribu kumuokoa mbwa wa  mwajiri wake mnamo siku ya Jumanne wiki jana, Desemba 12, 2024. Habari kuhusu kufariki kwake zilifikishwa kwa familia yake mnamo Desemba 14.

Kufuatia hayo, familia ya mwanariadha huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 36 ambayo inasemekana haijamwona kwa takriban miongo miwili sasa inaomba usaidizi wa kuleta mwili wake kutoka Mexico hadi nyumbani katika Kijiji cha Taabet, Chesoen, katika Kaunti ya Bomet kwa mazishi mwafaka.

Akizungumza na Nation, Bi Pauline Nowa, mamake marehemu mwanariadha huyo alifichua kwamba walihitaji takriban KSh 3 milioni ili kuuleta mwili huo nyumbani, lakini hawana kiasi hicho cha pesa.

Mjane wa Ngetich, Bi Janeth Ngetich alisema kwamba ni maelezo machache tu kuhusu kifo chake ambayo yamefichuliwa kwao.

“Kufikia sasa, taarifa tulizonazo ni kwamba alianguka ndani ya bwawa alipokuwa akijaribu kumwokoa mbwa aliyeingia kwa kasi kwenye kidimbwi cha maji. Alizama na mwili wake umehamishwa hadi katika chumba cha kuhifadhia maiti ukisubiri kufanyiwa uchunguzi,” aliomboleza Janeth Ngetich.

Wanafamilia walifichua kwamba marehemu aliondoka nchini Oktoba 27, 2007, wakati mkewe alipokuwa anatarajia mtoto wao, na kwamba alikuwa hajarejea tangu wakati huo.

“Aliwahi kukaa nje ya nchi kwa takribani miezi sita, ambapo alishiriki mbio mbalimbali kabla ya kurejea nyumbani kwa angalau miezi miwili na kupanda ndege tena. Huo ndio ulikuwa utaratibu hadi mwaka 2007, alipoondoka na hakurudi tena,” alisema Janeth.

Hata hivyo alisema kuwa marehemu alikuwa akiwasiliana na wanafamilia wake kwa simu na mara nyingi alikuwa akipiga nao simu za video akiwa na uhakika kwamba atarejea hivi karibuni.

Marehemu Josphat alistaafu takriban miaka 14 iliyopita baada ya kupata jeraha la mguu mwaka wa 2006. Jeraha hilo halikupona vya kutosha kumruhusu kuanza tena mashindano.