"Nilikosa usingizi siku 3 kuelekea Tokyo Marathon" Eliud Kipchoge afunguka baina ya machozi

"Nilipokea maneno mengi kwamba wataharibu na kuchoma biashara zangu mjini, nyumba yangu, familia…hiyo ndio ilikuwa habari mbaya kabisa katika maisha yangu,” Kipchoge alieleza.

Muhtasari

• “Katika [mbio za marathon za] Tokyo, nilikuwa na siku 3 bila usingizi, usiku na mchana. Sijui pahali usingizi ulienda, lakini sikuweza kulala,” Kipchoge alisema.

• Mkongwe huyo wa mbio za masafa marefu mwenye umri wa miaka 39 alieleza baina ya machozi kwamba alisikitishwa sana na mambo yaliyokuwa yakiendeshwa mitandaoni kwamba alihusika na kifo cha Kiptum.

Mwanariadha mzoefu katika mbio za masafa marefu.
Eliud Kipchoge// Mwanariadha mzoefu katika mbio za masafa marefu.
Image: Screengrab//BBC SPORT

Mwanariadha wa masafa marefu, Eliud kipchoge kwa mara ya kwanza amefunguka sababu zilizoathiri matokeo yake katika mbio za Tokyo Marathon mapema mwezi Machi.

Katika mbio hizo, Kipchoge aliweka rekodi mbaya kabisa katika historia yake ya kushiriki mbio za masafa marefu ambapo alimaliza wa 10.

Akizungumza na BBC Sport kuelekea mashindano ya Olympic jijini Paris Ufaransa kuanzia Julai, Kipchoge alisema kwamba alikosa usingizi siku chache kuelekea Tokyo Marathon, kutokana na maneno mengi ambayo alikuwa akiyasikia mitandaoni, jina lake likihusishwa na kifo cha Kelvin Kiptum aliyefariki Februari kwa ajali ya barabarani.

“Katika [mbio za marathon za] Tokyo, nilikuwa na siku 3 bila usingizi, usiku na mchana. Sijui pahali usingizi ulienda, lakini sikuweza kulala,” Kipchoge alisema.

Mkongwe huyo wa mbio za masafa marefu mwenye umri wa miaka 39 alieleza baina ya machozi kwamba alisikitishwa sana na mambo yaliyokuwa yakiendeshwa mitandaoni kwamba alihusika katka kifo cha marathoner mwenza ambaye awali alikuwa amevunja rekodi yake, Kiptum.

Katika mahojiano hayo, Kipchoge alisema kwamba kila kitu kilichojiri kipindi cha kifo cha Kiptum kilimpa funzo kubwa kutoamini mtu yeyote karibu naye, ikiwa ni pamoja na kivuli chake mwenyewe.

“Kilichotokea kusema kweli kimenifanya kuweka nadhiri ya kutoamini mtu yeyote. Hata kivuli changu mwenyewe sikiamini. Watu katika mitandao ya kijamii walikuwa wanasema kwamba Eliud alihusika katika kifo cha huyu kijana, nilipokea maneno mengi kwamba wataharibu na kuchoma biashara zangu mjini, nyumba yangu, familia…hiyo ndio ilikuwa habari mbaya kabisa katika maisha yangu,” Kipchoge alieleza.