'Niliogopa sana,'Kipchoge afichua tukio la kuhuzunisha baada ya kifo cha Kiptum

"Nilianza kuwapigia simu watu wengi, niliogopa sana," Kipchoge alisimulia.

Muhtasari
  • Kashfa hizo za mtandaoni ziliongezeka haraka, huku vitisho vikilengwa tu kwa Kipchoge bali pia kwa familia na mali yake ya kibinafsi.
alimaliza wa sita katika Boston Marathon.
Kipchoge alimaliza wa sita katika Boston Marathon.
Image: TWITTER// ELIUD KIPCHOGE

Mwanariadha wa mbio za marathoni wa rekodi ya dunia Eliud Kipchoge aliangua kilio alipofunguka tukio la kuhuzunisha baada ya uvumi kuanza kutanda kwenye mitandao ya kijamii unaodaiwa kumhusisha na kifo cha mwanariadha mwenzake Kelvin Kiptum.

Akiongea wakati wa mahojiano na BBC Sports, Kipchoge alidai alipokea vitisho vya kuuawa kutoka kwa watumiaji mtandaoni, jambo ambalo mshindi huyo wa medali ya dhahabu mara mbili katika Olimpiki alidai lilimtia hofu kubwa.

Mwanariadha huyo alisimulia kupokea jumbe kadhaa zikiwemo vitisho vilivyolenga familia yake na hata taaluma yake.

Kipchoge alipokuwa akisimulia matukio ya mateso nyumbani kwake mjini Eldoret, alilemewa na hisia.

“Mitandao yote ya kijamii ilikuwa ikidai, “Eliud alihusika katika kifo cha kijana huyu.” Nilipokea mambo mengi mabaya,” Eliud alifichua.

Kulingana na Kipchoge, jibu lake la kwanza alipopokea jumbe hizo za kuudhi ilikuwa kuangalia familia yake.

Akisimulia tukio hilo, mwanariadha huyo alipuuzilia mbali ripoti zinazomhusisha na kifo cha Kiptum. "Haijatokea lakini hivyo ndivyo ulimwengu ulivyo," Kipchoge alibainisha.

"Nilianza kuwapigia simu watu wengi, niliogopa sana," Kipchoge alisimulia.

Bingwa huyo mara mbili wa Olimpiki alifichua kwamba alilazimika kusimamisha shughuli kadhaa za familia kama tahadhari ya usalama.

"Nilishangaa watu kwenye mitandao ya kijamii wakisema 'Eliud anahusika katika kifo cha kijana huyu. Hizo zilikuwa habari mbaya zaidi kuwahi kutokea maishani mwangu," Kipchoge alisema.

Kashfa hizo za mtandaoni ziliongezeka haraka, huku vitisho vikilengwa tu kwa Kipchoge bali pia kwa familia na mali yake ya kibinafsi.

"Nilipata mambo mengi mabaya; kwamba watachoma kambi ya mafunzo, watachoma vitega uchumi vyangu mjini, watachoma nyumba yangu, watateketeza familia yangu," alisema.

Kipchoge aliambia BBC Sports kwamba walichagua kutofuata hatua za kisheria, na kutanguliza usalama wa wapendwa wake.

Kiptum alifariki pamoja na kocha wake Mnyarwanda katika ajali ya barabarani kando ya barabara ya Elgeyo Marakwet-Ravine mnamo Februari 11, 2024.