Kenya kuandaa mchujo wa kufuzu kwa Olimpiki Juni 14 na 15

Jumla ya wanariadha 270 wamealikwa kushindania nafasi katika timu ya Kenya ugani Nyayo Juni 14 na 15

Muhtasari

•Chama cha riadha nchini Kenya kimetoa orodha ya wanariadha watakaoshiriki kwenye jaribio ugani Nyayo ili kuteua watakaowakilisha Kenya kule Paris kwenye michezo ya olimpiki.

•Kila mwanariadha anayeelekea kwenye majaribio lazima awe na angalau jaribio moja la nje ya mashindano kati ya Septemba 4, 2023 na Mei 3, 2024.

Image: X @athleticsKenya

Wanariadha wa Kenya wanasubiri kwa hamu na gamu mchujo wa kitaifa utakaofanyika  kuanzia Juni 14 hadi  15  kuchagua kikosi kitakachowakilisha Kenya katika michezo ya Olimpiki ya Paris 2024.

 Paul Mutwii ambaye ni makamu wa rais wa chama cha riadha alisema wanariadha 49 wamefuzu kwa Olimpiki na wamethibitishwa kufuatia zoezi kali linalozingatia kufuzu kwa haki na kuwa wameadhimisha vigezo vilivyowekwa vya kupinga matumizi ya dawa za kusisimua misuli.

 Ferdinand Omanyala  anayeshiriki mbio za mita 100 na Zablom Ekwam wa mita 400 ndio wanariadha  pekee ambao wamefuzu kwa  mashindano ya Olimpiki Paris ya mwaka huu.

Miongoni mwa wanariadha walioalikwa ni mshikilizi wa rekodi ya dunia na bingwa wa Olimpiki wa mita 1500, Faith Kipyegon, ambaye atashiriki mbio za mita 1,500 na 5,000.

Kwenye mbio za  mita 400 wanaume ,Were, atashindana dhidi ya Moitalel Mpoke, Peter Kithome na Mbevi huku mbio za wanawake zikiongozwa na Jane Chege na Vanice Nyagisera.

Moraa pia amealikwa kwa mbio za mita 800 ambapo atamenyana na  Nelly Chepchirchir, Sarah Moraa, Naomi Korir na Vivian Kiprotich.

Mbio za mita 800 kwa wanaume zitahusisha  Emmanuel Wanyonyi,ambaye atashindana na Aaron Kemei, Wycliffe Kinyamal, Alex Ngeno, Emmanuel Korir na Ferguson Rotich.

Aidha, chama cha riadha pia  kimewaalika wanariadha kutoka Botswana, Uganda na Sudan Kusini kuongeza kasi ya mashindano hivyo kuongeza uwezekano wa kuongeza idadi.