Fedha ya Faith Kipyegon yarejeshwa baada ya rufaa iliyofaulu

Kipyegon alikuwa amepokonywa ushindi wa fedha baada ya kudaiwa kumsukuma Gudaf Tsegay wa Ethiopia.

Muhtasari

•Kipyegon alimaliza wa pili katika mbio za mita 5000 lakini akapokonywa ushindi kwa madai ya kumsukuma Gudaf Tsegay wa Ethiopia.

•Timu ya Kenya ilikata rufaa ili uamuzi wa kumuondoa Kipyegon kwenye mashindano utupiliwe mbali, na kwa bahati nzuri, rufaa ilifanikiwa.

alidaiwa Gudaf Tsegay.
Faith Kipyegon alidaiwa Gudaf Tsegay.
Image: HISANI

Rufaa iliyofaulu iliyofanywa na timu inayowakilisha Kenya katika Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024 imerudisha afueni kwa bingwa wa riadha Faith Kipyegon na mamilioni ya mashabiki wa Kenya wanaofuatilia mashindano ya kimataifa yanayoendelea nchini Ufaransa.

Siku ya Jumatatu usiku, mshindi huyo wa rekodi ya mbio za mita 1500 kwa wanawake alimaliza nambari mbili katika mbio za mita 5000 lakini akaondolewa katika mashindano kwa madai ya kumsukuma Gudaf Tsegay wa Ethiopia. Hii ilivunja sio tu moyo wa mwanariadha huyo, bali pia ya mamilioni ya mashabiki ambao walikuwa wakimtazama kote ulimwenguni.

Hatua hiyo ya kusikitisha hata hivyo haikumaanisha mwisho kwani maafisa wa timu ya Kenya walikata rufaa ili uamuzi wa kumuondoa Kipyegon kwenye mashindano utupiliwe mbali, na kwa bahati nzuri, rufaa ilifanikiwa.

"Rufaa iliyofanikiwa ilifanywa na #TeamKenya. Medali ya Fedha ya Faith wa ajabu ilirejeshwa," Timu ya Kenya ilisema katika taarifa usiku wa kuamkia Jumanne.

"Atakuwa amesimama karibu na Beatrice tunapoimba Wimbo wa Taifa kesho. Fedha ya mita 5000 ni ya Faith Kipyegon,” waliongeza.

Bingwa wa rekodi ya dunia ya mbio za mita 10,000, Beatrice Chebet alishinda medali ya kwanza ya dhahabu ya Kenya katika Michezo ya Olimpiki ya Paris katika mbio za mita 5,000 kwa wanawake baada ya kuibuka na ushindi wa dakika 14:28.56 Jumatatu usiku katika uwanja wa Stade de France.

Mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za mita 1,500, Faith Kipyegon aliibuka wa pili kwa dakika 14:29.60 lakini mwanzoni alikuwa amepokonywa ushindi baada ya kudaiwa kumsukuma Gudaf Tsegay wa Ethiopia.

Sifan Hassan wa Uholanzi aliibuka wa tatu baada ya kumaliza kwa muda wa dakika 14:30.61 na kutwaa shaba. Nadia Battocletti wa Italia (14:31.64) alishika nafasi ya nne Mkenya mwingine katika mbio hizo Margaret Chelimo aliwekwa wa tano (14:31.64).