Omanyala amevunja kimya baada ya kushindwa kufuzu fainali ya mita 100 kwenye Olimpiki

“Chochote unachokabili sasa - sio mwisho wa hadithi yako. Mungu yu pamoja nawe na atakuwa daima. Asante kwa kila mtu anayeamini kwamba hadithi ya Kenya haitakuwa kawaida tena,” Omanyala aliandika.

Muhtasari

• Mwanariadha huyo alimaliza wa mwisho katika mbio za nusu fainali hivyo hivyo kushindwa kujikatia tikiti ya kuingia kwenye fainali.

Mwanariadha wa Kenya Ferdinand Omanyala amevunja kimya chake siku moja baada ya kushindwa kufuzu kwenye fainali ya mbio za mita 100 katika mashindano ya Olimpiki yanayoendelea jijini Paris, Ufaransa.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Omanyala alidokeza kwamba anachokipitia katika maisha yake kwa sasa ni wakati mgumu sana lakini akakiri kwamba anafahamu fika kuwa yote ni mipango ya Mungu.

Mwanariadha huyo aliwashukuru Wakenya ambao walimsherehekea licha ya kushindwa kufuzu kwenye fainali, akisema kwamba ana uhakika historia ya Kenya kwenye mbio za mita 100 haitakuwa ya kawaida tena bali itabadilika.

“Chochote unachokabili sasa - sio mwisho wa hadithi yako. Mungu yu pamoja nawe na atakuwa daima. Asante kwa kila mtu anayeamini kwamba hadithi ya Kenya haitakuwa kawaida tena,” Omanyala aliandika.

Mwanariadha huyo alimaliza wa mwisho katika mbio za nusu fainali hivyo hivyo kushindwa kujikatia tikiti ya kuingia kwenye fainali.

Fainali hizo zilishuhudia mbio zaidi ambapo washiriki wote walifika utepeni kwa sekunde 10 kiasi kwamba iliwabidi waandaaji kuamua mshindi kwa kutumia utaalamu wa picha.

Mmarekani Noah Lyles alishinda mbio hizo, na kumaliza ngoja-ngoja ya miaka 20 ya Marekani kupata ubingwa wa mita 100 kwenye Olimpiki.

Licha ya matokeo ya Omanyala yasiyoridhisha, Wakenya wengi walimhongera kwa kupeperusha bendera ya Kenya katika mbio hizo ambazo miaka ya nyuma zilikuwa zinajulikana kama za mataifa mengine.

“Amina. Maji zaidi kwa kikombe chako. Daima uendelee kuwa mwanga. Tunakushukuru kaka” Bien Aime Sol alimwambia.

“Bado ulitufanya tujivunie! Kuendelea na juu,” Mwanahabari Larry Madowo alisema.

“MFALME!!! Kesho ni yako,’ King Kaka.