Ijumaa jioni, mwanariadha wa Kenya Beatrice Chebet alikimbia na kushinda na kujinyakulia dhahabu yake ya pili katika Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024.
Chebet alishinda mbio za mita 10,000 za wanawake, akimaliza mbele ya Nadia Battocletti wa Italia na nyota wa Uholanzi Sifan Hassan ambao walishinda fedha na shaba mtawalia.
Alikimbia hadi kwenye mstari wa kumalizia kwa muda wa 30:43.25 ili kudai nafasi yake juu ya jukwaa, na kutwaa taji la Olimpiki mbele ya umati wa mashabiki waliokuwa wakishangilia kwenye uwanja wa Stade de France.
"Nina furaha sana, kushinda mbio za mita 5000 na 10,000 si jambo rahisi," Chebet alisema baada ya mbio hizo.
"Lakini zingatia tu, na ujue kuwa unaweza kufanikiwa, jiamini tu. Niliamini kuwa ningeweza. Nilitaka tu kushinda mbio za mita 10,000 kwa nchi yangu. Nchi yangu haijawahi kushinda medali ya dhahabu (katika mbio za 10,000 za wanawake." m). Kwa hivyo nilisema nilitaka kuwa mwanamke wa kwanza kushinda medali ya dhahabu katika mbio za mita 10,000," aliongeza.
Zaidi, Chebet alisema ushindi huo ni wa Wakenya wote na akawashukuru kwa sapoti kubwa ambayo wamempa.
"Ninatoa medali hii kwa Wakenya wote. Nataka tu kusikia nchi yangu inajivunia. Hii ilikuwa kwa ajili yenu, mlikuwa akilini na moyoni mwangu katika kila mzunguko, ningeweza kuwa nimeweka historia lakini nitalala vyema nikijua Wananchi wataenjoy wikendi," alisema.
Mapema wiki hii, Bingwa huyo wa riadha alishindia Kenya dhahabu nyingine katika mbio za mita 5000 kwa wanawake.