"Marathoni mbaya zaidi!" Kipchoge azungumza baada ya kuondoka uwanjani, kushindwa kukamilisha mbio

Bingwa huyo alidondoka kwenye uwanja wakati wa mbio baada ya kukimbia kwa zaidi ya nusu ya safari.

Muhtasari

•Kipchoge amekiri wazi kwamba mbio za Jumamosi mjini Paris  ndizo mbio zake za marathoni mbaya zaidi kuwahi kutokea.

•Alisema atafikiria kuhusu hatua yake inayofuata, akidokeza anaweza kuwa anafunga miongo yake miwili ya mbio za kitaaluma.

wakati wa marathoni ya Olimpiki ya Paris
Eliud Kipchoge wakati wa marathoni ya Olimpiki ya Paris
Image: HISANI

Mshindi wa dhahabu ya Olimpiki mara mbili, Eliud Kipchoge, wa Kenya amekiri wazi kwamba mbio za Jumamosi mjini Paris  ndizo mbio zake za marathoni mbaya zaidi kuwahi kutokea.

Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 39 ambaye ameshinda medali nyingi katika miongo miwili iliyopita alijiondoa katika mbio na kushindwa kukamilisha mwendo katika Olimpiki ya Paris inayoendelea baada ya kukimbia nusu ya safari.

Akizungumza baada ya mbio hizo za kukatisha tamaa, alibainsiha kuwa katika miaka yake 21 ya kukimbia, hajawahi kukosa kukamilisha mbio kama alivyofanya leo.

"Ni wakati mgumu kwangu. Hii ni marathon yangu mbaya zaidi. Sijawahi kufanya DNF (kukosa kumaliza). Hayo ndiyo maisha. Kama bondia, nimeangushwa, nimeshinda, nimeshika nafasi ya pili, ya nane. , 10, tano - sasa sikumaliza," Kipchoge alisema.

Akizungumzia mipango yake ya baadaye, alisema atafikiria kuhusu hatua yake inayofuata, akidokeza kwamba anaweza kuwa anafunga miongo yake miwili ya mbio za kitaaluma.

"Hayo ndiyo maisha...sijui nini kitakachofuata. Nahitaji kurejea [nyumbani], kuketi chini, kujaribu kufikiria miaka yangu 21 ya kukimbia katika kiwango cha juu. Ninahitaji kubadilisaha na kushiriki katika mambo mengine," Alisema.

Jumamosi asubuhi, Kipchoge alikosa nafasi ya kuwa mwanariadha wa kwanza katika historia kushinda medali tatu za dhahabu za marathoni katika mashindano hayo.

Bingwa huyo wa marathon hakuweza kuendana na kasi ya washindani wake katika nusu ya safari wakati wa mbio za marathon za Olimpiki ya Paris Jumamosi asubuhi, na kuua ndoto yake ya kuwa bingwa kwa mara ya tatu mfululizo. Alishikilia nafasi ya 63 baada ya kukimbia kwa kilomita 25 ya mbio hizo za 42km.

Tamirat Tola wa Ethiopia alifika ukingoni baada ya saa 2:06.26, na kuvunja rekodi ya Olimpiki na pia kupata dhahabu ya kwanza ya nchi yake katika michezo hiyo.

Mwanariadha wa Ubelgiji Bashit Abdi (2.06.47) alimaliza wa pili na kutwaa medali ya fedha, huku Mkenya Benson Kipruto akishinda shaba kwa kutumia saa 2:07:00.

Kipchoge alikuwa anatazamia kuwa mwanariadha wa kwanza kushinda mataji matatu ya marathon katika michezo hiyo.