Hellen Obiri azungumza baada ya kushindia Kenya medali ya 11 katika Olimpiki ya Paris

Katika taarifa yake, Obiri alibainisha kuwa Kenya imefunga Olimpiki kwa medali 11.

Muhtasari

• Obiri amewashukuru Wakenya kwa sapoti ambayo wamewapa timu inayowakilisha taifa kwenye Michezo ya Olimpiki ya Paris.

•Timu ya Kenya imeleta nyumbani dhahabu nne,  fedha mbili, na shaba tano.

akikimbia katika Paris Olympics
Hellen Obiri akikimbia katika Paris Olympics
Image: TEAM KENYA

Mshindi wa nishani ya shaba katika mbio za marathon za wanawake Hellen Obiri amewashukuru Wakenya kwa sapoti ambayo wamewapa timu inayowakilisha taifa kwenye Michezo ya Olimpiki ya Paris.

Katika taarifa yake Jumapili asubuhi baada ya kuibuka nambari tatu katika mbio za marathon za Olimpiki za Paris kwa wanawake, Obiri alibainisha kuwa Kenya imefunga Olimpiki kwa medali 11.

"Ni medali ya shaba. Mbio zetu kwenye Olimpiki zimekamilika na tumemaliza na medali 11 kwa jumla. Asante Kenya kwa sapoti yako kubwa," Obiri alisema kupitia mtandao wa kijamii wa X.

Jumapili asubuhi, Obiri alikamilisha mbio za kilomita 42 kwa muda wa saa 2.23.10, nyuma ya Sifan Hassan wa Uholanzi (2.22.55) na Tigist Asefa wa Ethiopia (2.22.58) na kushindia  Kenya medali ya kumi na moja katika mashindano hayo.

Mkenya mwingine, Sharon Lokedi aliibuka wa nne baada ya kukimbia kwa saa 2.2314, akikosa medali kwa sekunde chache tu.

Obiri na Lokedi walipambana vikali na walikuwa wakiongoza pamoja kwa muda mrefu katika kilomita za mwisho za mbio hizo kabla ya Hassan na Asefa kuwazidi nguvu katika takriban mita mia mbili za mwisho.

Shaba katika mbio za marathon za wanawake sasa inafikisha jumla ya medali za shaba zilizoshindwa na Wakenya katika Michezo ya Olimpiki ya Paris hadi tano.

Timu ya Kenya pia imeleta nyumbani dhahabu nne, na fedha mbili.

Medali za dhahabu zilinyakuliwa na Beatrice Chebet katika mbio za mita 5000 na 10000 kwa wanawake, Faith Kipyegon katika mbio za mita 1500 kwa wanawake, na Emmanuel Wanyonyi katika mbio za mita 800 kwa wanaume.

Faith Kipyegon pia alishinda nchi hiyo medali ya fedha katika mbio za mita 5000 kwa wanawake huku Ronald Kwemoi akishinda medali hiyo katika mbio za mita 5000 kwa wanaume.

Mary Moraa (mbio za mita 800 za wanawake), Faith Cherotich (mbio za mita 3000 kwa wanawake kuruka viunzi), Abraham Kibiwot (mbio za mita 3000 kuruka viunzi wanaume), Benson Kipruto (Mbio za Marathon za Wanaume), na Hellen Obiri aliyeibuka wa tatu katika mbio za wanawake marathon waliletea Kenya medali za shaba.