Mshindi wa dhahabu katika mbio za mita 3000 kuruka viunzi kwa wanawake kwenye Michezo ya Olimpiki ya Paris, Winfred Yavi amerejea nyumbani nchini Kenya.
Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 24 aliiwakilisha Bahrain katika Michezo ya Olimpiki ya 2024 licha ya kuzaliwa katika kaunti ya Makueni nchini Kenya. Amekuwa akiwakilisha taifa hilo la Mashariki ya Kati kwa takriban miaka minane iliyopita tangu abadilishe kutoka Kenya.
Video ya kipindi cha kihisiawakati mwanariadha huyo mahiri alipokuwa akipokelewa katika uwanja wa ndege na wapendwa wake siku ya Jumanne kwa sasa inavuma kwenye mitandao ya kijamii.
Katika video hiyo, Yavi anaonekana akionyesha medali yake ya dhahabu kwa wapendwa wake waliokusanyika huku wazazi wake wakisimama kando yake.
Bingwa huyo wa Olimpiki alionekana kuzidiwa na hisia huku akipigwa picha na hata alionekana akijifuta machozi ya furaha yaliyokuwa yakitiririka mashavuni mwake. Kwa kweli, ilikuwa ni wakati mzuri na wa kihemko kwake na kwa familia yake alipoonyesha ushindi wake.
Haya yanajiri siku chache tu baada ya mwanariadha huyo mahiri mwenye umri wa miaka 24 kuwasilisha medali yake kwa mfalme wa Bahrain Hamad bin Isa Al Khalifa katika ikulu ya taifa hilo.
Siku ya Jumapili, Yavi, alielezea furaha yake alipokuwa akikabidhi nishani yake ya dhahabu kwa mfalme Hamad bin Isa Al Khalifa.
Katika picha alizoonyesha, alionekana akionyesha medali ya kifahari ambayo alishinda katika michezo ya hivi majuzi ya Olimpiki ya Paris kwa mfalme alipotembelea ikulu.
Alisema kuwa pia alipata nafasi ya kuzungumza na mfalme kuhusu matukio ya nchini Ufaransa na akamshukuru kwa sapoti yake kwa wanariadha.
"Ilikuwa heshima kuonyesha matukio yetu katika Michezo ya Olimpiki na medali kwa Mfalme wake Hamad bin Isa Al Khalifa. Tunashukuru sana kwa uungwaji mkono wa Ukuu wake, " Yavi alisema.
Mwanariadha huyo aliyezaliwa katika kaunti ya Makueni alishinda medali ya dhahabu katika mbio za mita 5000 kuruka viunzi na maji kwa wanawake katika mashindano ya Paris OIympics 2024 yaliyokamilika.
Katika mahojiano ya awali, Yavi alisema kabla ya kufanya uamuzi wa kuhamia Bahrain takriban miaka nane iliyopita, alifanya majaribio mengi ili kupata nafasi katika timu ya taifa ya Kenya lakini hakufanikiwa kwani kulikuwa na ushindani mkali.
"Nilikuwa nikienda kwa majaribio ya timu ya Kenya, na sikufuzu. Kuenda Bahrain kilikuwa kipaumbele cha kwanza, lakini nilikuwa tayari kuwakilisha nchi yangu,” Yavi alisema.
Aliongeza, "Ushindani ulikuwa mkali. Unajua hapa Kenya tuko na wanariadha wengi na pia kupata ile nafasi angalau uingie kwa timu ya Kenya, ndio unaweza kuingia kwa timu ya Kenya lakini unapata wanachagua watu wawili tu, kama wewe ni nambari mbili ama nne unakosa. Mimi nilikuwa tayari kabisa lakini nilikuwa nakosa nafasi.”