logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Ndoto ya Omanyala kung'aa kwenye Mashindano ya Dunia ya Oregon yatatizwa

Omanyala alikosa kusafiri pamoja na wanariadha wengine wa Kenya siku ya Jumatatu.

image
na Radio Jambo

Yanayojiri13 July 2022 - 07:02

Muhtasari


•Omanyala amefichua kwamba bado yupo nchini Kenya kwa kukosa VISA licha ya kuwa mashindano ya mbio za mita 100 yatafanyika siku ya kwanza.

•Kundi la kwanza la wanariadha wa Kenya liliondoka nchini Jumatatuu usiku  kuelekea Marekani kwa ajili ya maandalizi.

Ferdinand Omanyala

Ferdinand Omanyala ni mwenye wasiwasi kufuatia kucheleweshwa kwa Visa yake ya usafiri  huku zikiwa zimesalia siku mbili tu kabla ya Michuano ya Dunia ya Oregon kuanza.

Mashindano ya Oregon World Championship 2022  yatang'oa nanga Ijumaa, Julai 15 na kuendelea kwa wiki nzima  hadi Jumapili, Julai 24. Yataendelea katika mji wa Eugene, jimbo la Oregon huko Marekani.

Omanyala amefichua kwamba bado yupo nchini Kenya kwa kukosa VISA licha ya kuwa mashindano ya mbio za mita 100 yatafanyika siku ya kwanza.

"Inasikitisha kuwa sijasafiri hadi Oregon bado na mbio za mita 100 ni baada ya siku mbili. Ucheleweshaji wa visa," Omanyala alisema kupitia Instagram.

Jumatatu bingwa huyo wa mbio za mita 100 alikosa kusafiri pamoja  na wanariadha wengine wa Kenya watakaoshiriki mashindano ya Oregon.

Kundi la kwanza la wanariadha wa Kenya liliondoka nchini Jumatatuu usiku  kuelekea Marekani kwa ajili ya maandalizi.

Meneja wa timu hiyo Rono Bunei alieleza kuwa wanariadha  wangesafiri kwa makundi kulingana na tarehe za mashindano yao husika.

"Seti ya kwanza ya wanariadha itaondoka leo (Jumatatu) usiku wa kuamkia leo. Tumepiga kambi katika uwanja wa Moi, Kasarani kwa wiki mbili zilizopita na ninaamini wanariadha wetu watatoa matokeo mazuri," Bunei alisema Jumatatu.

Omanyala anatazamia kushiriki mbio za Oregon kwa mara ya kwanza mwaka huu. Lengo lake kuu katika mashindano hayo ni kuvunja rekodi ya Afrika.

"Umbo langu la sasa ni la sekunde 9.6 na kuendelea lakini ubingwa ukishindwa kwa sekunde  9.55 hadi sekunde 9.60 basi nitainua mikono yangu. Hakika nitashinda ikiwa kasi itakuwa sekunde 9.66 kwenda sekunde 9.70," Omanyala alisema katika mahojiano na Nation.

Bingwa huyo ndiye anayeshikilia rekodi ya Afrika katika mbio za mita 100 (sekunde 9.77), rekodi ambayo aliweka Septemba mwaka jana katika mashindano ya  Kip Keino Classic Tour yaliyofanyika jijini Nairobi.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved