Omanyala avunja kimya baada ya kubanduliwa nje ya Mashindano ya Dunia huko Oregon

Omanyala ,26, alimaliza katika nafasi ya tano baada ya kukimbia kwa sekunde 10.14.

Muhtasari

•Omanyala ,26, alimaliza katika nafasi ya tano baada ya kukimbia kwa sekunde 10.14 na hivyo akakosa kufuzu kwa fainali.

•Omanyala ameweka wazi kwamba hatakata tamaa na ataendelea kupambana zaidi katika mbio hizo licha ya changamoto ambazo zimekumba safari yake.

akishiriki mashindano ya dunia huko Oregon
Bingwa wa Afrika katika mbio za mita 100 Ferdinand Omanyala akishiriki mashindano ya dunia huko Oregon
Image: TWITTER// FERDINAND OMANYALA

Bingwa wa Afrika katika mbio za mita 100 Ferdinand Omanyala hatashiriki katika fainali za mbio hizo kwenye michuano ya riadha ya dunia inayoendelea Oregon, Marekani.

Hii ni baada ya mwanariadha huyo mwenye kipaji kikubwa kubanduliwa nje katika hatua ya nusu fainali usiku wa  kuamkia Jumapili.

Omanyala ,26, alimaliza katika nafasi ya tano baada ya kukimbia kwa sekunde 10.14 na hivyo akakosa kufuzu kwa fainali.

Akizungumza baada ya matokeo hayo ya kuvunja moyo, Omanyala aliweka wazi kwamba hatakata tamaa na ataendelea kupambana zaidi katika mbio hizo licha ya changamoto ambazo zimekumba safari yake.

"Kila changamoto unayokutana nayo leo inakufanya uwe na nguvu kesho. Changamoto ya maisha imekusudiwa kukufanya kuwa bora, sio uchungu. Ustahimilivu na uvumilivu huja tu kwa kupewa nafasi ya kushughulikia shida ngumu. Haijalishi ni kiasi gani kinachoanguka juu yetu, tunaendelea kusonga mbele," Bingwa huyo alisema kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Awali siku ya Jumamosi staa huyo wa mbio za mita 100 aliwasisimua Wakenya baada ya kufuzu kwa nusu fainali licha ya kuwasili Marekani masaa machache tu kabla ya mashindano ya makundi kung'oa nanga.

Omanyala ambaye alikimbia katika kundi la saba alimaliza wa tatu  kwa sekunde 10.10 na hivyo kujikatia tiketi kushiriki nusu fainali.

Safari yake ya kuelekea Marekani ilitatizika kufuatia kucheleweshwa kwa Visa yake ya usafiri. Alipata stakabadhi hiyo muhimu Alhamisi kisha kuanza safari na kuwasili Oregon  takriban masaa matatu tu kabla ya mashindano ya kufuzu semi fainali za mbio za mita 100 kung'oa nanga.

Omanyala ana maono makubwa. Ndoto yake kubwa imekuwa kuvunja rekodi ya Usian Bolt wa Jamaica na kuandikisha rekodi mpya ya dunia.

Mwaka jana mwanariadha huyo alivunja rekodi ya Afrika na kuandikisha rekodi mpya ya 9.77 alipokimbia katika michuano ya Kip Keino Classic iliyofanyika Nairobi.