Omanyala kukosa mashindano ya riadha ya dunia nchini Marekani kufuatia kuchelewa kwa Visa

Alithibithisha kupitia kwa msemaji wake kwamba hatashiriki mashindano hayo

Muhtasari

•Kufikia Jumatano mwanariadha huyo matata hakuwa amekata safari yake kuelekea jimbo la Oregon, Marekani.

•Omanyala alithibithisha kupitia kwa msemaji wake kwamba hatashiriki mashindano hayo kwa kuwa hakupokea visa yake kwa wakati mzuri wa kusafiri.

Ferdinand Omanyala
Ferdinand Omanyala
Image: HISANI

Ni rasmi kwamba bingwa wa Afrika katika mbio za mita 100 Ferdinand Omanyala hatashiriki kwenye mashindano yajayo ya World Athletics Championships kufuatia kuchelewa kwa Visa yake ya kusafiri.

Kufikia Jumatano mwanariadha huyo matata hakuwa amekata safari yake kuelekea jimbo la Oregon, Marekani ambako mashindano hayo yatafanyika kati ya Ijumaa wiki hii na Jumapili wiki ijayo.

Ripoti ya Reuters imesema Omanyala alithibithisha kupitia kwa msemaji wake kwamba hatashiriki mashindano hayo kwa kuwa hakupokea visa yake kwa wakati mzuri wa kusafiri.

"Cha kusikitisha, sitashiriki katika mashindano ya dunia ya mwaka huu huko Oregon. Sikupata visa yangu kwa wakati wa kusafiri," Omanyala alisema kupitia msemaji wake.

Hapo awali mwanariadha huyo alikuwa ameeleza wasiwasi wake kuhusu ukosefu wa  stakabadhi hiyo muhimu ya usafiri.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Omanyala alifichua kwamba bado yupo nchini licha ya siku ya mashindano kuwa karibu.

"Inasikitisha kuwa sijasafiri hadi Oregon bado na mbio za mita 100 ni baada ya siku mbili. Ucheleweshaji wa visa," Omanyala alisema kupitia Instagram.

Akizungumza na kituo kimoja cha Redio cha hapa nchini, mwanariadha huyo alithibitisha kuwa bado alikuwa akifanya mazoezi yake ugani Kasarani huku akisubiri Visa.

Jumatatu bingwa huyo wa mbio za mita 100 alikosa kusafiri pamoja  na wanariadha wengine wa Kenya watakaoshiriki mashindano ya Oregon.

Kundi la kwanza la wanariadha wa Kenya liliondoka nchini Jumatatuu usiku  kuelekea Marekani kwa ajili ya maandalizi.

Meneja wa timu hiyo Rono Bunei alieleza kuwa wanariadha  wangesafiri kwa makundi kulingana na tarehe za mashindano yao husika.

"Seti ya kwanza ya wanariadha itaondoka leo (Jumatatu) usiku wa kuamkia leo. Tumepiga kambi katika uwanja wa Moi, Kasarani kwa wiki mbili zilizopita na ninaamini wanariadha wetu watatoa matokeo mazuri," Bunei alisema Jumatatu.