Picha ya kutia huruma ya bondia Conjestina Achieng imezua gadhabu mitandaoni

Muhtasari

• Picha ya bondia wa zamani wa kike Conjestina Achieng imezua gadhabu mitandaoni huku baadhi wakilaumu wizara ya michezo kwa kumtelekeza.

Bondia Conjestina Achieng
Image: Stephen Mukangai (Facebook)

Picha za kuhuzunisha za bondia wa zamani wa kike Conjestina Achieng zimevunja ukimya katika mitandao ya kijamii ambapo watu wengi wameashiria kugadhabishwa kwao na hali ya kutia huruma ya mwanamasumbwi huyo wa zamani wa Kenya.

Kwa kuwa wengi wana misemo yao kwamba picha huzungumza maneno zaidi ya elfu, basi ni kweli kwa hali ambayo Achieng anaonekana kutia huruma kwa picha ni ishara tosha isiyohitaji maelezo zaidi kwamba mwanandondi huyo anapitia wakati mgumu sana katika maisha yake.

Picha hiyo ambayo imesambazwa katika mtandao wa Facebook inamuonyesha Conjestina Achieng akiwa ameshikilia mlango wa gari na mkono wa mtu asiyefahamika ukiwa kama unamuelekeza kuingia garini vile, huku uso wa Achieng ukiwa hauna furaha wala tabasamu kabisa – kwa asilimia kubwa tu uso wake unaonekana kujawa na mapeto, ishara ya kuwa na hali ngumu kimaisha na pengine msongo wa mawazo.

Wengi waliotoa maoni yao kwenye picha hiyo isiyo na furaha waliilaumu srikali kuu na serikali ya kaunti anakotoka mwanamasumbwi huyo wa zamani, haswa wizara ya michezo kwa kumtelekeza Achieng kwa muda mrefu na kusahau sifa zote alizolimbikizia taifa enzi za ubora wake katika ulingo wa mviringo kupambana katika mchezo wa ngumi.

“PICHA ya Kuvunja MOYO sana ya Aliyekuwa Bondia Nguli Conjestina Achieng katika mitaa ya Siaya. Hii inavunja moyo sana. Kuna serikali ya County na kuna wizara ya michezo Kenya hii. Lakini kwa nini?” aliandika kwa gadhabu kubwa mtangazaji na mchanganuzi wa masuala ya kispoti Stephen Mukangai kwenye ukurasa wake wa Facebook ambapo pia alipakia hiyo picha.

Ikumbukwe miaka kadhaa iliyopita bondia huyo wa zamani alisemekana kudhoofika afya ya akili ambapo wadau mbalimbali walijitokeza na kuahidi kusimamia matibabu yake katika kituo cha kurekebisha tabia na kushughulikia afya ya akili ambapo haijulikani ilienda vipi baada ya kusemekana kwamba ameshapona na kuruhusiwa kurudi zake nyumbani.

Lakini kwa muda mrefu sasa hali yake imekuwa ikitiliwa shaka iwapo kweli alipona kabisa kutokana na matatizo hayo ya afya ya kiakili ambapo picha zake akiwa katika hali duni zikiibua maswali mengi kuliko majibu yake.

Watu walitofautiana wazi katika mtandao huku baadhi wakiilaumu serikali na wizara ya michezo huku kukiwa na mrengo mwingine unaomlaumu Conjestina Achieng kwa kutumia mapato yake visivyo enzi nyota yake ilipokuwa angavu.

“Nina aibu kuwa Mkenya, viongozi wetu wizara ya michezo, huyu alileta utukufu kwa taifa letu. Unyogovu una tibika,” mmoja aliandika

“Kwa kadiri tunavyowalaumu viongozi wetu, wanamichezo wetu pia wanapaswa pia kutumia vyema siku zao wakati wapo katika hali shwari kimichezo ili kujiepusha na mambo kama haya wakati hawapo tena ulingoni,” aliandika mwingine.