Conjestina Achieng kuwafundisha mabondia chipukizi baada ya kutoka kwenye rehab

Bondia huyo wa zamani amekuwa rehab kwa miezi minane.

Muhtasari

•Katika taarifa yake ya Jumatano, Radull alifichua kwamba kwa sasa hali ya mama huyo wa kijana mmoja imeimarika.

•Radull alifichua kwamba bondia huyo wa zamani atakuwa na kibarua cha kuwafunza wacheza ndondi chipukizi.

Maendeleo ya Bondia Conjestina Achieng
Image: HISANI

Mchanganuzi wa spoti Carol Radull ametoa taarifa kuhusu maendeleo ya bondia wa zamani Conjestina Achieng', takriban miezi minane baada ya kupelekwa katika kituo cha kurekebisha hali jijini Mombasa.

Lejendari huyo wa ndondi alipelekwa katika kituo cha Mombasa Women Empowerment Network mwaka jana kwa ufadhili wa aliyekuwa gavana wa Nairobi, Mike Sonko, baada ya kukumbwa na matatizo ya kiakili.

Katika taarifa yake ya Jumatano, Radull alifichua kwamba kwa sasa hali ya mama huyo wa kijana mmoja imeimarika.

"Miezi nane katika kituo cha Mombasa na msichana wangu Conjestina Achieng anakaa vizuri!" alisema kwenye Instagram.

Mchanganuzi huyo wa spoti aliendelea kufichua kwamba baada ya kukamilisha kipindi chake cha matibabu katika kituo hicho, Bi Conjestina atakuwa na kibarua cha kuwafunza wacheza ndondi chipukizi.

"Kazi kwenye gym inamngoja baada ya kukamilisha ambapo atakuwa akiwafunza mabondia wadogo," Radull alisema.

Kufuatia hayo, alitoa shukrani za dhati kwa Mike Sonko kwa niaba ya bondia huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Kenya.

Sonko alimpeleka bondia huyo wa zamani katika kituo cha kurekebisha hali cha Women Empowerment Network mwezi Julai mwaka jana baada ya kukutana na familia ili kujadili mikakati ya matibabu yake.

Katika mkutano huo, mfanyibiashara huyo aliahidi kulipia gharama zote za hospitali za bondia huyo hadi atakapopata nafuu.

"Tutakuwa naye mpaka mwisho. Haijalishi itachukua muda gani. Mradi niko hai na Mungu amenipatia uwezo nitafika mwisho na Conje," Alisema.

Mwezi Septemba, Conjestina alilazimika kujitokeza kuzima tetesi kwamba ameaga dunia baada ya habari feki kusambazwa.

Wakati huo, bondia huyo wa zamani aliweka wazi kwamba alikuwa sawa na alikuwa anaendelea vyema na  matibabu.

"Mimi naendelea vizuri. Kila kitu kiko sawa. Naendelea na matibabu. Wale watu walikuwa wakisema eti nimekufa, sijafa niko sawa," aliwaambia wanahabari.

Bingwa huyo wa ndondi aliwasuta watu ambao walikuwa wakieneza uvumi kuwa amefariki baada ya afya yake kudhoofika.

Alisema kwa sasa yuko vizuri zaidi na hata anafanya mazoezi katika juhudi za kurejea kwenye ulingo wa ndondi hivi karibuni.

"Watu wajaribu kuchunga ulimi. Wakati wanaposema kitu wanafaa kujua maana yake kabla ya kusema," Alisema