Mandonga, Wanyonyi wapeana vitisho vikali kabla ya kumenyana Julai

Wanandondi hao watamenyana katika pambano bila ubingwa katika mtaa wa Westlands, Nairobi mnamo Julai 22.

Muhtasari

• Mandonga ameratibiwa kurejea nchini akiwa na azimio la kumuangamiza mpinzani wake mkubwa Daniel Wanyonyi.

• Wanyonyi, bingwa wa zamani wa ndondi za Afrika (ABU) aliapa kutumia pambano hilo kujikomboa baada ya kupigwa vibaya awali.

Bondia maarufu Mondonga
Bondia maarufu Mondonga
Image: INSTAGRAM// KARIM MANDONGA

Bondia Mtanzania Karim ‘Mtu Kazi’ Mandonga ameratibiwa kurejea nchini akiwa na azimio la kumuangamiza mpinzani wake mkubwa Daniel Wanyonyi.

Wanandondi hao watamenyana katika pambano bila ubingwa linalosubiriwa kwa hamu katika ukumbi wa Sarit Expo Centre, katika mtaa wa Westlands, Nairobi Julai 22.

Baada ya kumshinda mpinzani wake wa Kenya mjini Nairobi kwa ngumi yake maarufu ya "Sugunyo" inayodaiwa kutoka Ukraine, Mandonga sasa ameahidi kuleta kombora jipya lililobatizwa jina la "Kikuki" kutoka Urusi katika mchuano wao ujao.

Mabondia hao wawili walibadilishana cheche kabla ya pambano halisi linaloandaliwa na kuahidi kuwapa mashabiki wao mechi ya ndondi ya hali ya juu siku ya pambano.

“Nimerejea nchini Kenya kuthibitisha taji langu kama bondia bora zaidi Afrika Mashariki. Nilimwacha Wanyonyi akiwa na uso ulioharibika katika pambano letu la mwisho na nimerudi kumzika akiwa hai mara moja,” Mandonga alisema.

“Sijali anachosema. Nitamharibu apende asipende,” Mandonga aliongeza.

Katika majibu yake, Wanyonyi, bingwa wa zamani wa ndondi wa Afrika (ABU) aliapa kutumia pambano hilo kujikomboa baada ya kupigwa vibaya awali, na kuahidi kuonyesha ustadi katika pambano hilo la raundi kumi.

"Ikiwa anafikiria kuwa atakuwa na mechi rahisi kama alivyofanya kwenye pambano letu la mwisho basi atapigwa na butwa. Wakati huu hatanusurika kupita awamu ya kwanza,” Wanyonyi alisema.

"Mara ya mwisho, ulinipata nikiwa na kutu baada ya janga la Covid-19 nchini ulininyima fursa ya kufanya mazoezi ili kujitayarisha kwa vita vyetu. Mambo ni tofauti kabisa sasa na nimegundua upya fomu yangu halisi. Atakuwa akikabiliana na mnyama aliyejeruhiwa,” Wanyonyi aliongeza.

Wanyonyi, 39, alishindwa na Mandonga kupitia TKO katika raundi ya tano ya pambano lao kali lililofanyika katika jumba la kongamano la KICC.

Mkenya huyo anaingia kwenye pambano hilo akiwa amejiamini kufuatia pambano lake la hivi punde zaidi ambapo alimpiga Charles Kakande wa Uganda kwa TKO kwenye Uwanja wa Kasarani mnamo Machi 25.

Lakini anakabiliana na mpinzani mkali ambaye amewahi kumshida kwa njia sawa Lucky Yamuzi wa Uganda katika uwanja huo huo,siku hiyo hiyo.