Mandonga afurahia kipigo Kenya, kuzichapa tena na Mganda Jumamosi hii

Bondia huyo mkazi wa Morogoro anatarajiwa kupanda tena ulingoni kuzichapa na Mganda Moses Golola.

Muhtasari

• " Siku ya leo naona ilikua bahati yake kunaliza raundi tu ndio bahati yake lakini hakuna siku nakosea, kwa sababu kama nakosea angenipiga KO(Knockout), mimi nmempiga yule KO," Mandoga.

•Jaji George Athmani alimpa Wanyonyi alama 100-80, Jaji Wycliffe Marende 100-80, na Jaji Leonard Wanga 100-89.

Image: BBC

Bondia mwenye mbwembwe na tambo nyingi Karim Mandonga wa Tanzania amesema anafurahia matokeo ya pambano lake la mwishoni mwa wiki dhidi ya Daniel Wanyonyi wa Kenya licha ya kupoteza pambano hilo.

Akizungumza na NTV ya Kenya mara baada ya Pambano hilo Mandonga alisema " Siku ya leo naona ilikua bahati yake kunaliza raundi tu ndio bahati yake lakini hakuna siku nakosea, kwa sababu kama nakosea angenipiga KO(Knockout), mimi nmempiga yule KO".

Mandonga akaongeza " kwa hiyo mimi hakuna la kukosea naona mchezo ndivyo ulivyo, ukimaliza kuna matokeo matatu suluhu, kushinda au kushindwa, kwa hiyo mimi nimekubaliana na matokeo yalitokea leo (usiku wa kuamkia Julai 23,2023), nmefurahi sana kwa hiyo, ila tuangalie rematch (pambano la marudiano), tuone nini kinaendelea, ndani ya Kenya".

Katika Mapambo hilo la raundi 10 uzani wa Light heavyweight lililofanyika jijini Nairobi usiku wa kuamkia Julai 23,2023, Majaji wote watatu walimpa Wanyonyi ushindi.

Jaji George Athmani alimpa Wanyonyi alama 100-80, Jaji Wycliffe Marende 100-80, na Jaji Leonard Wanga 100-89.

Hili ni Pambano la pili kwa mabondia hao wa Afrika Mashariki kukutana, pambano la kwanza lililofanyika Januari 2023 huko huko Nairobi, Mandonga alimchapa Wanyonyi.

Wakati huo huo Julai 29,2023 Bondia huyo mkazi wa Morogoro anatarajiwa kupanda tena ulingoni kuzichapa na Mganda Moses Golola

Pambano hilo kwenye Usiku wa Vitasa litafanyika jijini Mwanza akiwa na ngumi mpya inayoitwa Ndukube.

Mandonga anasema ukipigwa ngumi hiyo kwa mkono wa kulia unageuka kichuguu na ukipigwa kwa mkono wa kushoto unapata fangasi.