Klabu ya Arsenal imethibitisha kujiuzulu kwa Mkurugenzi wake wa Michezo Edu Gaspar.
Katika taarifa ya Jumatatu jioni, klabu hiyo yenye maskani yake jijini London ilimshukuru mchezaji huyo wake wa zamani ambaye alichukua nafasi ya mkurugenzi wa michezo takriban miaka mitano iliyopita kwa huduma yake na kumtakia kila la heri katika hatua yake ifuatayo.
Aidha, walikiri kwamba Mbrazil huyo alikuwa muhimu sana katika utekelezaji wa mkakati mpya wa soka na alisaidia kuipeleka klabu mbele.
"Edu Gaspar leo amejiuzulu wadhifa wake kama Mkurugenzi wetu wa Michezo. Edu, mchezaji wetu wa zamani na Invincible, alijiunga nasi tena katika nafasi ya Mkurugenzi wa Ufundi mnamo Julai 2019. Aliendelea na klabu na akapandishwa cheo na kuwa Mkurugenzi wa Michezo mnamo Novemba 2022, ambapo alisimamia soka la wanaume, wanawake na akademi,” Arsenal ilisema katika taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti rasmi.
Taarifa hiyo ilisomeka zaidi, “Tunamshukuru Edu kwa mchango wake katika mkakati wetu mpya wa soka na kuipeleka klabu mbele akiwa na maadili ya Arsenal moyoni mwake.”
Huku akizungumzia kujiuzulu kwake, Edu alikiri kwamba uamuzi wake wa hivi punde haukuwa rahisi kufanya.
Aliwashukuru wamiliki wa klabu hiyo kwa kupata nafasi ya kuitumikia na kueleza kuwa wakati umefika kwake kufanya kitu tofauti.
"Arsenal imenipa fursa ya kufanya kazi na watu wengi wa ajabu na nafasi ya kuwa sehemu ya kitu maalum katika historia ya klabu," alisema.
"Nimependa kufanya kazi na wenzangu wengi wakubwa katika timu zetu za wanaume, wanawake na wasomi, haswa Mikel, ambaye amekuwa rafiki mkubwa. Sasa ni wakati wa kutafuta changamoto tofauti. Arsenal itabaki moyoni mwangu daima. Naitakia klabu na wafuasi wake mambo mema tu na kila la kheri,” alisema.
Wamiliki wa klabu hiyo walikiri kwamba wanaheshimu uamuzi wa Edu wa kujiuzulu na kumtakia heri katika safari iliyo mbele yake.