Mkondo wa nne wa michuano ya klabu bingwa barani Ulaya
umekuwa mzito kwa timu za Uingereza baada ya matokeo ya kutoridhisha kurekodiwa
Jumanne na Jumatano usiku.
Uingereza inawakilishwa na timu za Liverpool, Manchester
City, Aston Villa na Arsenal na kati ya timu
hizi, ni Liverpool pekee iliyovuna ushindi katika mechi za mkondo wa nne kwenye
ligi hiyo.
Jumanne usiku, mabingwa mara nne mfululizo wa ligi ya
Uingereza Manchester City walipoteza kwa Sporting CP mabao manne kwa moja
ugenini huku Liverpool wakiandikisha ushindi muhimu wa mabao manne kwa nunge
dhidi ya Bayer Leverkusen ya Ujerumani.
Ugumu kwa timu za Uingereza kuandikisha matokeo mazuri yaliendelea
Jumatano uaiku huku wakati Aston Villa na Arsenal wakipoteza kwa kunyoroshwa
bao moja kwa kavu kila mmoja.
Club Brugge ikiwa nyumbani iliilambisha vumbi Aston Villa
kupitia bao la mchezaji Hans Vanaken la penalti katika dakika ya 52 ya mchezo.
Masaibu ya Arsenal yaliwapata dakika za nyongeza kabla ya mapumziko kwa Inter
Milan kupata penalti baada ya mpirfa kumpiga Mikel Merino mkononi.
Kufikia sasa, ikiwa inasalia mechi nne za kubaini timu
zitakazofuzu moja kwa moja kwa hatua inayofuata kwa kumaliza katika nane bora, Liverpool
inashikilia nafasi ya kwanza kwa alama 12 baada ya ushindi wa mechi zote nne
ikiimarisha fursa ya kufuzu moja kwa moja.
Aston Villa ipo katika nafasi ya nane kwa alama tisa baada
ya kupoteza mechi moja dhidi ya Club Brugge Jumatano usiku.
Man City na Arsenal wanashikilia nafasi ya 10 na 12 mtawalia
kwa alama saba kila mmoja na ikiwa watamaliza katika na nafasi kati ya 9 na 24,
watalazimika kucheza mechi za maondoano moja ya nyumbani na nyingine ya ugenini
ili kufuzu hatua ya mbele.