logo

NOW ON AIR

Listen in Live

75% ya vilabu vya EPL wanataka City ishushwe daraja - Pep Guardiola azungumzia mashtaka 115 ya Man City

Hukumu dhidi ya City itatolewa kati ya Februari na Machi mwaka ujao.

image
na Samuel Mainajournalist

Football23 November 2024 - 12:05

Muhtasari


  •  Pep alibainisha kuwa klabu nyingi za Ligi Kuu ya Uingereza zinataka Man City iadhibiwe kwa kushushwa daraja.
  •  Meneja huyo alidokeza kuwa atakubali uamuzi wowote utakaotolewa dhidi yao.


Meneja wa Manchester City Pep Guardiola amesisitiza kujitolea kwake kwa klabu hiyo hata wakati wanasubiri hukumu ya mashtaka 115 dhidi yao.

 City walishtakiwa na kutumwa kwa tume huru mnamo Februari 2023 kufuatia uchunguzi wa miaka minne. Inadaiwa walikiuka sheria zake za kifedha kati ya 2009 na 2018.

 Wakati akizungumza na waandishi wa habari siku ya Ijumaa, kabla ya mechi ya Jumamosi dhidi ya Tottenham, kocha huyo mwenye umri wa miaka 53 alieleza imani yake kwa klabu hiyo na kuweka wazi kuwa anapanga kusalia bila kuzingatia hukumu itakayotolewa mapema mwaka ujao.

 Pep alibainisha kuwa klabu nyingi za Ligi Kuu ya Uingereza zinataka Man City iadhibiwe kwa kushushwa daraja kutoka ligi kuu.

 "Nilisoma kitu kuhusu jinsi tunavyohitaji kushushwa daraja mara moja. Asilimia 75 ya vilabu vinataka hilo, kwa sababu najua wanachofanya nyuma ya pazia na aina hii ya mambo," Pep Guardiola alisema.

 Aliongeza, "Napendelea kutokuwa katika nafasi hiyo lakini ikishafika naipenda - kwa sababu unaamini katika klabu yako na watu wa huko. Ninaamini wanachoniambia [kuhusu madai ya ukiukaji] na sababu kwa nini. Tunasubiri hukumu mwezi Februari au Machi.”

 Meneja huyo alidokeza kuwa atakubali uamuzi wowote utakaotolewa dhidi yao na akabainisha kuwa washindi hao wa EPL 2023/24 bado watapanda tena iwapo watashushwa daraja.

 "Itakuwaje tukishuka daraja? mimi nitakuwa hapa, sijui nafasi watakayotuletea, Conference? Lakini tutapanda na kurejea Ligi Kuu, nahisi, "alisema.

 Huku ikiwa bado ikiwa imesalia miezi michache kabla ya uamuzi dhidi ya City, lengo la haraka la klabu ni kuwania ubingwa wa Ligi Kuu kulingana na Guardiola.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved