Meneja wa Manchester City Pep Guardiola amekiri kuwa klabu hiyo iko katika hali mbaya kufuatia kipigo cha aibu dhidi ya Tottenham Hotspurs siku ya Jumamosi.
City walipokea kipigo cha 0-4 kutoka kwa vijana wa Ange Postecoglou siku ya Jumamosi usiku na kuashiria kushindwa kwao kwa tano mfululizo katika mashindano yote.
"Katika miaka minane, hatujawahi kuwa katika hali ya aina hii. Sasa tunapaswa kustahimili na kuivunja kwa kushinda michezo ijayo, hasa ijayo. Sasa tunaona mambo kwa njia moja, labda katika wiki chache tunaona tofauti,” Guardiola alisema baada ya mechi.
Hata hivyo, alionyesha imani yake kubwa kwamba watarejea katika njia za ushindi baada ya kipindi kibaya wanachopitia.
“Tutarudi tena, Tutafanya hivyo,” alisema.
Akizungumzia mechi dhidi ya Spurs iliyoisha kwa kipigo cha aibu, meneja huyo mwenye umri wa miaka 53 alikiri kwamba walikuwa duni katika safu ya ulinzi.
"Katika wakati huu sisi ni dhaifu katika ulinzi. Tulianza vizuri kama kawaida, lakini hatukuweza kufunga na baada ya hapo tukakubali. Baada ya hapo tulikubali zaidi jambo ambalo ni gumu kwa hisia zetu hivi sasa,” alisema.
Kocha huyo wa zamani wa Bayern Munich pia alikiri kwamba kushindwa na Spurs kumepunguza nafasi yao ya kushinda EPL 2024/25 akibainisha kuwa vinara wa ligi hiyo Liverpool wako katika hali nzuri, hivyo basi wanaifanya vigumu kuwapata.
Pep alipoulizwa kama klabu yake bado ina nafasi ya kushinda tena taji hilo, alisema, "Sijui. Lakini hatufikirii kama tutashinda au kupoteza [taji la EPL]. Hatuko tayari kufikiria kitakachotokea mwishoni mwa msimu.
Aidha, alidokeza kuwa kwa sasa wanalenga kushinda michezo ijayo, na kufuzu kwa hatua inayofuata ya Ligi ya Mabingwa.
"Mwishowe ikiwa hatutashinda taji ni kwa sababu hatustahili - tuliposhinda hapo awali ni kwa sababu tunastahili. Tunachopaswa kufanya sasa ni Feyenoord [Jumanne]. Hilo ndilo jambo muhimu zaidi - kwanza kwa kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa - na hatua kwa hatua wachezaji watakuwa bora," Pep alisema.
Mabao mawili kutoka kwa James Maddison na moja moja kutoka kwa Pedro Porro na Brennan Johnson Jumamosi jioni yaliiwezesha City kushindwa kwa mara ya kwanza nyumbani katika mechi 52, na kipigo kikubwa zaidi nyumbani tangu kuchapwa 5-1 na Arsenal mnamo 2003.