Meneja wa Manchester City Pep Guardiola amethibitisha kujitolea kwake katika klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza licha ya matokeo hafifu ya hivi majuzi.
Guardiola hivi majuzi aliongeza mkataba wake katika klabu ya Man City kwa angalau misimu mingine miwili lakini hatua hiyo iliambatana na hali mbaya ya kikosi chake.
Ingawa meneja huyo anayesifiwa sana anakubali, hana kinga ya kufutwa kazi, anasema hana majuto juu ya kuongeza mkataba wake hadi msimu wa joto wa 2027.
Guardiola alisema hana mpango wa kuondoka klabuni hiyo huku akibainisha kuwa anaweza kujutia mengi iwapo ataondoka.
“Nitajuta kama ningeondoka sasa. Ningelala vibaya zaidi kuliko sasa. Haiwezekani kuacha hali kama ilivyo sasa," Guardiola alisema katika mkutano wake na waandishi wa habari.
Aliongeza, "Wanaweza kunifuta. Hilo linaweza kutokea tukiendelea hivi lakini tukiondoka sasa, hakuna nafasi. Kama bosi wangu, Khaldoon [Al Mubarak] hajafurahishwa na mimi, wanaweza kufanya hivyo, lakini sasa kuondoka katika nafasi hiyo, hakuna nafasi."
Guardiola hata hivyo alibainisha kuwa endapo atalazimishwa kuondoka klabuni hapo, ataondoka kwa fahari, baada ya kupata mafanikio mengi huko tayari.
“Nikiona ni muda wa kuondoka nitaondoka vizuri, ningesema lengo la kunifanya maisha yangu au safari yangu ya hapa au muda wangu wa hapa uwe tofauti kabisa, haiwezekani, nikiondoka kesho au nikiondoka kidogo... nimekuwa bora katika klabu hii, sitawahi kusahau, sisubiri hadi nishinde Ligi Kuu nyingine au Ligi ya Mabingwa, hapana.”
Guardiola alizungumza kabla ya mechi inayosubiriwa kwa hamu ya Manchester Derby ambayo itachezwa kwenye Uwanja wa Etihad Jumapili jioni.
Mechi hiyo inazikutanisha timu mbili ambazo zimekuwa kwenye hali isiyotabirika hivi karibuni, zikiwa na matumaini ya kupata pointi ili kuepuka kushuka ngazi kwenye jedwali la Ligi Kuu.
Man
City kwa sasa wapo nafasi ya tano wakiwa na pointi 27 huku Man United wakishika
nafasi ya 13 wakiwa na pointi 19.