Kiungo
wa Tottenham, Rodrigo Bentancur alitolewa nje kwa machela baada ya kucheza dakika
sita tu za mechi ya Jumatano ya nusu fainali ya Kombe la Carabao dhidi ya
Liverpool.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uruguay mwenye umri wa miaka 27 alianguka chini bila kutegwa au kusukumwa alipokuwa akijinyoosha kupiga mpira wa kona kwa kichwa.
Kiungo huyo alipotua chini, alibaki kuwa mtulivu, jambo lililozua wasiwasi wa haraka miongoni mwa wachezaji wa timu zote mbili.
Madaktari walipewa ishara haraka kushughulikia hali hiyo, na kusababisha kusimamishwa kwa mchezo kwa takriban dakika 10.
Uzito wa tukio hilo ulithibitishwa wakati Bentancur alipohitaji oksijeni uwanjani kabla ya kusogezwa kwa uangalifu kwenye nafasi ya kuketi kwa tathmini zaidi.
Muda mrefu wa kusimamishwa kwa mechi ulihitimishwa kwa mchezaji huyo kubebwa nje kwa machela huku mashabiki wakipiga makofi kote uwanjani.
Tottenham baadaye ilichapisha sasisho kwenye akaunti yao ya X, ikisema: "Tunaweza kuthibitisha Rodrigo yuko na fahamu, anazungumza na atakwenda hospitali kwa uchunguzi zaidi."
Alitibiwa uwanjani kwa takriban dakika tisa kabla ya nafasi yake kuchukuliwa na fowadi Brennan Johnson.
Kocha wa Tottenham, Ange Postecoglou aliiambia Sky Sports baada ya mchezo kumalizika: "Sina taarifa zote. Ninachoelewa ni kwamba ana fahamu na alikuwa na fahamu alipofika chumba cha kubadilishia nguo. Tulimpeleka hospitali ili kuchunguzwa.
"Ilikuwa ya kutia wasiwasi na kila mara ilikuwa ya wasiwasi lakini kutokana na kile ninachojua ninatumai atakuwa sawa."
Mchuano uliochezwa kwenye Uwanja wa Tottenham Hotspur ulimalizika kwa bao 1-0 kwa Spurs baada ya Lucas Bergvall kufunga bao la dakika za mwisho.