Kocha wa Arsenal Mikel Arteta amedokeza kuhusu klabu hiyo kusajili mshambuliaji katika dirisha la usajili la Januari ambalo bado lipo wazi.
Akizungumza na vyombo vya habari siku ya Jumanne, Mhispania huyo mwenye umri wa miaka 42 alisema wana mawazo wazi kuhusu aina ya mshambuliaji ambaye anataka kumsajili katika Arsenal.
Wanabunduki tayari wamekuwa wakiwinda kwa ajili ya kuimarisha mashambulizi, lakini juhudi hizo zimeongezeka kufuatia jeraha la goti la Gabriel Jesus.
Mbrazil huyo hivi majuzi alipata jeraha la ACL katika goti lake la kushoto, na atafanyiwa upasuaji siku zijazo, baada ya kubebwa nje kwa machela wakati Arsenal iliposhindwa na Manchester United kwenye Kombe la FA Jumapili.
Alipoulizwa kama ana wazo kuhusu aina gani ya mshambuliaji angependa kuleta, Arteta alisema: "Tuna mawazo ya wazi kabisa ya wachezaji tunaowataka, ndiyo."
"Ilikuwa kabla ya Gabi kujeruhiwa, na vile Gabi alivyojeruhiwa hivi sasa na tunapaswa kusubiri na kuona jinsi mambo yanavyoendelea," aliongeza.
Aliposukumwa kufichua ni aina gani ya mchezaji anatafuta, Arteta alisema: "Unaweza kuzungumza na [mkurugenzi wa muda wa michezo] Jason [Ayto]. Unajua sitazungumza kuhusu hilo.”
Kumpoteza Jesus ni pigo kubwa kwa Arsenal kwani tayari hawana fowadi mwenzake Bukayo Saka hadi angalau Machi.
Saka alijeruhiwa kwenye msuli wa paja kwenye mechi iliyochezwa
Crystal Palace mwezi uliopita na, baada ya kufanyiwa upasuaji, atakuwa nje kwa
miezi kadhaa.
"Ni wazi tunapoteza wachezaji wawili wabunifu sana,
muhimu sana, wasiotabirika sana kwetu, kwa hivyo hiyo ina athari kwa timu. Hiyo
ni hakika, " Arteta alisema.
"Sio kwa sasa, ni tangu mwanzo wa dirisha na kabla ya dirisha tulikuwa tukiangalia kwa dhati nini tunaweza kufanya kupanga na kuboresha kikosi, kuathiri kikosi, ikiwa tunaweza," alisema.
Wanabunduki watacheza dhidi ya Tottenham Hotspurs katika mechi inayosubiriwa kwa hamu ya London Derby Jumatano jioni. Watakuwa wanataka kupata pointi tatu ili kupunguza pengo kati ya Liverpool walio nafasi ya kwanza.