Klabu ya soka ya Manchester United imeonyesha nia ya kutaka kumsajili
mchezaji mwingine chipukizi kutoka Arsenal baada ya kufanya mawasiliano na beki
Ayden Heaven kuhusu uwezekano wa kumnunua.
Mwandishi wa habari za soka wa kuaminika Fabrizio Romano mnamo Alhamisi jioni alifichua kwamba Man United imefanya mawasiliano na Wanabunduki kuhusu uwezekano wa kumsajili beki huyo wa kati mwenye umri wa miaka 18.
Mhitimu huyo wa akademi ya Arsenal anachezea timu ya taifa ya Uingereza ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 19 na tayari ameshacheza kwa mara ya kwanza katika klabu hiyo yenye maskani yake London. Alicheza katika mashindano ya Kombe la Carabao msimu uliopita.
Mkataba wa Heaven unaisha mnamo 2025 na kijana huyo anavutia vilabu vingi vikubwa.
Eintracht Frankfurt ya Ujerumani na Barcelona ya Uhispania pia zimeripotiwa kufanya mawasiliano na kinda huyo.
Wanabunduki pia wanataka kuhifadhi mhitimu huyo wa Hale End lakini hawana meni ya kusema kwani mkataba wake unatarajiwa kumalizika baada ya miezi sita.
Heaven amewahi kuichezea England katika kiwango cha Under-18 na Under-19.
Beki huyo amepitia akademi ya vijana ya Gunners lakini United wameweka historia ya kunyakua vipaji vya vijana wa Arsenal, baada ya hapo awali kumpata Chido Obi-Martin kutoka klabu hiyo ya kaskazini mwa London.
Heaven hata inaripotiwa kuwa katika Uwanja wa Old Trafford wakati Man United ilipoilaza Rangers 2-1 katika mechi ya Ligi ya Europa Alhamisi jioni.
Haijabainika iwapo United wataweza kumsajili kinda huyo mwezi huu.
Iwapo United watamsajili, ni wazi kwamba hana uzoefu mkubwa wa kuwa bora papo hapo Old Trafford lakini ana uwezo wa kusukuma haraka mipango yake katika kikosi cha kwanza cha Ruben Amorim.
Mchezaji huyo wa miaka 18 ni beki wa kati anayetumia mguu wa kushoto - bidhaa adimu.
Huko United, ni Lisandro Martinez pekee ndiye anayetumia mguu wa kushoto na Muargentina huyo ameonekana kuyumba msimu huu.
Sasa inaonekana timu ya kuajiri ya United imekuwa ikifuatilia kwa karibu akademi ya Arsenal siku za hivi majuzi huku pia ikifanikiwa kumshawishi Chido Obi-Martin kuhamia Manchester mwaka jana.