logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Baada ya kuwa Man United miezi 2, ninahisi niko na miaka 50 sio 40 - Kocha Ruben Amorim akiri

Amorim amedai kwamba amezeeka kwa zaidi ya muongo mmoja tangu achukue mikoba ya Erik ten Hag katika Man United.

image
na Samuel Mainajournalist

Football27 January 2025 - 08:13

Muhtasari


  • Amorim ambaye anasherehekea siku ya kuzaliwa leo Jumatatu, alisema anahisi kama anatimiza miaka 50 badala ya 40 baada ya miezi miwili katika Man United.
  • Amorim pia alikiri kukataa ombi la wachezaji kuchukua mapumziko Jumatatu akisema watasherehekea siku yake ya kuzaliwa naye baada ya siku ya mazoezi.


Kocha mkuu wa Manchester United Ruben Amorim mnamo Jumapili usiku alitania kwamba amezeeka kwa zaidi ya muongo mmoja tangu achukue mikoba ya Erik ten Hag katika klabu hiyo.

Kocha huyo wa zamani wa Sporting Lisbon, ambaye anasherehekea siku yake ya kuzaliwa leo JumatatuJanuari 27, alisema anahisi kama anatimiza miaka 50 badala ya 40 baada ya miezi miwili ya kuwa Manchester United.

Mashetani wekundu walimpa Mreno huyo zawadi ya mapema kwa siku yake ya kuzaliwa kwa kupata ushindi wa 1-0 dhidi ya Fulham, shukrani kwa shuti lililopigwa na mlinzi Lisandro Martinez.

Ushindi huo ulikuwa wa nne pekee kwa Amorim kuonja mafanikio ya ligi tangu achukue mikoba kutoka kwa Erik ten Hag mnamo Novemba, huku mabingwa hao mara 20 wa ligi kuu wakiwa bado wanatatizika katikati mwa jedwali.

"Siyo 40… ninatimiza umri wa miaka 50. Baada ya miezi miwili nikiwa Manchester United ni miaka 50. Ni bahati nzuri kutimiza miaka 40 nikiwa hapa," Amorim aliambia BBC alipoulizwa kama ushindi wa Fulham ulikuwa zawadi nzuri ya siku ya kuzaliwa.

"Hisia hiyo ya kushinda na pointi tatu ni muhimu sana kwetu. Huwezi kuona maendeleo makubwa katika timu na huo ni ukweli. Lakini kushinda hutusaidia kuimarika,” aliongeza.

Amorim pia alikiri kukataa ombi la wachezaji kuchukua mapumziko Jumatatu akifichua kwamba watasherehekea siku yake ya kuzaliwa naye baada ya siku ya mazoezi.

"Waliomba siku ya mapumziko kesho, sikuwapa, kwa hivyo tunafanya mazoezi kwa sababu ni siku yangu ya kuzaliwa na zawadi yangu ni kufanya kazi na vijana ambao hawakucheza, itakuwa nzuri kwa sababu tumeshinda. kula chakula cha jioni na watoto wangu," alisema.

Kilikuwa ni kipigo cha kwanza cha Fulham katika uwanja wa Craven Cottage tangu Novemba 23 na Amorim alikiri kwamba ana deni kubwa la shukrani kwa Toby Collyer, 21, ambaye aliweka kibali cha hali ya juu kuwanyima wenyeji bao la kusawazisha dakika za mwisho.

"Alifanya hivyo kwa mazoezi wakati mmoja. Toby aliokoa timu yetu leo," alisema Amorim.

Mshindi wa mechi, Lisandro Martinez pia alijawa na sifa kwa mchezaji mwenzake, akisifu tabia ya unyenyekevu ya Collyer.

"Nadhani nilikuwa na bahati, lakini nimefurahishwa sana na jinsi tulivyoshinda mchezo. Haijalishi nani alifunga. Pointi tatu muhimu zaidi, jinsi tunavyopigana, jinsi tunavyocheza," Martinez alisema kwenye TNT Sports. .

 "Na jamaa huyu [Collyer]. Jamaa huyu ni mfano mzuri kwa kizazi kipya. Anafanya kazi kwa bidii na ni mnyenyekevu sana, anastahili yote," aliongeza.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved