logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Al Nassr Yazungumzia Madai Ya Duran Kulazimika Kusafiri Kutoka Bahrain hadi Saudia Kila Siku Ili Kuishi Na Mpenziwe

Klabu hiyo imeweka wazi kwamba Duran atakuwa akiishi katika nyumba ambayo iko karibu na uwanja wao.

image
na Samuel Mainajournalist

Football06 February 2025 - 07:55

Muhtasari


  • Al Nassr imekanusha vikali madai kwamba mshambuliaji wao mpya, Jhon Duran, analazimika kusafiri zaidi ya kilomita 500 kutoka Bahrain hadi Riyadh.
  • “Jhon anapenda Riyadh, na nyumba yake iko karibu na klabu na uwanja wetu. Yeye ni sehemu mpya ya familia yetu,” Al Nassr ilisema.

Jhon Duran Akiwa Al Nassr

Klabu ya Al Nassr imekanusha vikali madai kwamba mshambuliaji wao mpya, Jhon Duran, analazimika kusafiri zaidi ya kilomita 500 kutoka Bahrain hadi Riyadh ili kuwa karibu na mpenzi wake baada ya kuhamia Saudi Arabia.

Taarifa hizo zilianza kusambaa kwenye vyombo vya habari vya kimataifa, zikidai kwamba Duran ameamua kuishi Bahrain kwa sababu ya sheria za kihafidhina za Saudi Arabia zinazokataza wapenzi ambao hawajafunga ndoa kuishi pamoja.

Hata hivyo, Al Nassr sasa imevunja kimywa na kuyataja madai hayo kama "habari bandia za kuchekesha."

Wakati ikijibu moja ya akaunti iliyochapisha madai hayo kwenye X, klabu hiyo inayoshiriki Saudi Pro League iliweka wazi kwamba Duran atakuwa akiishi katika nyumba ambayo iko karibu na uwanja wao.

"Sote tumesikia kuhusu kile kinachoitwa 'habari bandia', lakini hii ni habari bandia ya kuchekesha sana! Tunafurahia kuona klabu yetu ina umuhimu mkubwa kiasi hiki 😄,” Al Nassr ilisema katika taarifa ya Jumatano jioni.

“Jhon anapenda Riyadh, na nyumba yake iko karibu na klabu na uwanja wetu. Yeye ni sehemu mpya ya familia yetu,” taarifa ilisoma zaidi.

Jhon Duran, ambaye alihamia Al Nassr hivi karibuni akitokea Aston Villa ya England, anatajwa kuwa moja ya wachezaji wenye vipaji vikubwa vya kizazi kipya.

Nyota huyo wa kimataifa wa Colombia ana matarajio makubwa ya kung'ara katika ligi ya Saudi Pro League, na anaonekana kuanza kuzoea maisha yake mapya nchini humo.

Licha ya uvumi ulioenea, ripoti zinaonyesha kuwa Duran anaishi Riyadh, karibu na uwanja wa mazoezi wa Al Nassr, jambo linalothibitisha kuwa hana haja ya kusafiri kati ya Bahrain na Saudi Arabia kama ilivyodaiwa.

Saudi Arabia ina sheria kali kuhusu uhusiano wa wanandoa ambao hawajafunga ndoa, lakini wachezaji wengi wa kigeni, wakiwemo nyota wakubwa kama Cristiano Ronaldo na Karim Benzema, wameweza kuishi na wake zao au wapenzi wao bila matatizo makubwa.

Hii inadhihirisha kuwa mamlaka zinaweza kutoa urahisi kwa wachezaji wa kimataifa kuhakikisha wanapata mazingira mazuri ya kuishi na kucheza soka kwa kiwango cha juu.

Al Nassr inatarajia kufanya vyema kwenye mashindano mbalimbali msimu huu, ikiongozwa na nyota kama Ronaldo, Sadio Mané, na sasa Jhon Duran.

Ujio wa mshambuliaji huyo kijana unaongeza nguvu kwenye kikosi cha kocha Luis Castro, huku klabu ikiendelea kuimarisha nafasi yake kama moja ya timu kubwa barani Asia.

Kwa kanusho hili rasmi kutoka kwa Al Nassr, ni wazi kuwa klabu hiyo haitaki uvumi na habari za uongo kuathiri mchezaji wao mpya au taswira yao kwa ujumla.

Mashabiki sasa wanangoja kuona Duran akifanya kazi uwanjani na kuonyesha thamani yake ndani ya jezi ya Al Nassr.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved