logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Marcelo: Gwiji Wa Brazil Na Real Madrid Atangaza Kustaafu Soka Akiwa Na Miaka 36

Marcelo ameeleza kuwa safari yake kama mchezaji imefika mwisho lakini bado ana mengi ya kutoa katika mchezo wa soka.

image
na Samuel Mainajournalist

Football06 February 2025 - 15:50

Muhtasari


  • Marcelo alianza safari yake ya soka katika klabu ya Fluminense nchini Brazil kabla ya kujiunga na Real Madrid mnamo mwaka 2007.
  • Marcelo anahesabiwa kama mmoja wa mabeki wa kushoto bora zaidi kuwahi kucheza mchezo wa soka.

Marcelo

Beki matata wa Brazil na klabu ya Fluminense, Marcelo Vieira da Silva Júnior, ametangaza kustaafu rasmi kutoka soka la kulipwa.

Kupitia ujumbe wa hisia kali aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii mnamo Alhamisi Februari 6, Marcelo alieleza kuwa safari yake kama mchezaji imefika mwisho lakini bado ana mengi ya kutoa katika mchezo wa soka.

"Hadithi yangu kama mchezaji inafikia tamati hapa. Lakini bado nina mengi ya kuchangia katika soka. Asanteni kwa kila kitu," aliandika Marcelo chini ya video yake ya kuaga mashabiki wake.

Marcelo, mwenye umri wa miaka 36, alianza safari yake ya soka katika klabu ya Fluminense nchini Brazil kabla ya kujiunga na Real Madrid mnamo mwaka 2007.

Alitumia misimu 16 akiwa na miamba hao wa Hispania, akishinda mataji 25, yakiwemo matano ya UEFA Champions League.'

Kwa mafanikio hayo, aliweka historia kama mmoja wa wachezaji waliotwaa mataji mengi zaidi katika klabu hiyo maarufu duniani.

Baada ya kuondoka Real Madrid mwaka 2022, Marcelo alijiunga kwa muda mfupi na Olympiacos ya Ugiriki, kisha akarudi Fluminense kwa msimu wake wa mwisho.

Mechi yake ya mwisho rasmi ilichezwa Oktoba 26, 2024, dhidi ya EC Vitória katika ligi ya Brazil.

Marcelo anahesabiwa kama mmoja wa mabeki wa kushoto bora zaidi kuwahi kucheza mchezo wa soka.

Alijulikana kwa kasi yake, uwezo wa kudhibiti mpira, mashambulizi makali kutoka pembeni, na ubunifu mkubwa uwanjani.

Katika timu ya taifa ya Brazil, alicheza jumla ya mechi 58, akiwakilisha taifa lake katika michuano mbalimbali, ikiwemo Kombe la Dunia.

Katika maisha yake ya soka, Marcelo ametwaa mataji 28 ya kimataifa, 25 kati ya hayo akiwa na Real Madrid. Kwa mchango wake mkubwa katika klabu hiyo, alitajwa kama mmoja wa viongozi wa kihistoria wa Madrid na hata kuvaa beji ya unahodha wa timu.

 Licha ya kuhitimisha safari yake kama mchezaji, Marcelo amesisitiza kuwa bado ana ndoto na mipango mikubwa katika soka. Ingawa hajaweka wazi atajihusisha vipi na mchezo huo, mashabiki wake wanatarajia kumuona akiendelea kutoa mchango mkubwa kwa kizazi kipya cha wanasoka.

Kustaafu kwa Marcelo ni mwisho wa enzi kwa mmoja wa mabeki wa kushoto waliopamba viwanja kwa ustadi wa hali ya juu.

Urithi wake utaendelea kuishi katika kumbukumbu za mashabiki wa Real Madrid, Brazil, na ulimwengu mzima wa soka.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved