logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Cristiano Ronaldo amwandikia Marcelo ujumbe wa kihisia kufuatia tangazo la kustaafu

Cristiano alitambua jinsi taaluma ya beki huyo wa kushoto wa Brazil imekuwa ya kuvutia na akamshukuru kwa mambo makubwa waliyofanya pamoja.

image
na Samuel Mainajournalist

Football07 February 2025 - 07:49

Muhtasari


  • Cristiano alimtakia kila la heri mchezaji mwenzake wa zamani katika klabu ya Real Madrid Marcelo anapochukua hatua ya kustaafu.
  • "Wewe ni zaidi ya mwenzangu, mshirika wa maisha yangu. Asante kwa kila kitu, rafiki. Nakutakia kila la kheri katika hatua hii mpya ya maisha” alisema.

Cristiano Ronaldo na Marcelo wakati wakiwa Real Madrid

Staa maarufu wa soka Cristiano Ronaldo mnamo siku ya Alhamisi alimtakia kila la heri rafiki yake wa muda mrefu na mchezaji mwenzake wa zamani katika klabu ya Real Madrid Marcelo Vieira da Silva Júnior anapochukua hatua ya kustaafu.

Marcelo alitangaza kustaafu kucheza soka ya kulipwa siku ya Alhamisi mchana katika video ya kihisia, na hivyo kuhitimisha taaluma yake ya soka ya takriban miongo miwili.

Katika ujumbe wake kwa Marcelo kupitia X, Cristiano alitambua jinsi taaluma ya beki huyo wa kushoto wa Brazil imekuwa ya kuvutia na akamshukuru kwa mambo makubwa waliyofanya pamoja.

“Ndugu yangu, ni taaluma ya ajabu kweli ambayo umekuwa nayo! Tulifanya mengi sana pamoja, na miaka ya mafanikio ya ushindi, na nyakati zisizoweza kusahaulika,” Ronaldo alimwandikia mchezaji mchezaji huyo wa zamani.

Nyota huyo wa Ureno ambaye kwa sasa anakipiga katika klabu ya Al Nassr ya nchini Saudi Arabia alizungumzia uhusiano mzuri uliopo kati yake na Marcelo na kumtakia mema katika harakati zake zijazo.

"Wewe ni zaidi ya mwenzangu, mshirika wa maisha yangu. Asante kwa kila kitu, rafiki. Nakutakia kila la kheri katika hatua hii mpya ya maisha” aliandika.

Beki Marcelo Vieira da Silva Júnior, alitangaza kustaafu rasmi kutoka soka la kulipwa siku ya Alhamisi Februari 6, 2025.

Kupitia ujumbe wa hisia kali aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii, Marcelo alieleza kuwa safari yake kama mchezaji imefika mwisho lakini bado ana mengi ya kutoa katika mchezo wa soka.

"Hadithi yangu kama mchezaji inafikia tamati hapa. Lakini bado nina mengi ya kuchangia katika soka. Asanteni kwa kila kitu," aliandika Marcelo chini ya video yake ya kuaga mashabiki wake.

Marcelo, mwenye umri wa miaka 36, alianza safari yake ya soka katika klabu ya Fluminense nchini Brazil kabla ya kujiunga na Real Madrid mnamo mwaka 2007.

Alitumia misimu 16 akiwa na miamba hao wa Hispania, akishinda mataji 25, yakiwemo matano ya UEFA Champions League.'

Kwa mafanikio hayo, aliweka historia kama mmoja wa wachezaji waliotwaa mataji mengi zaidi katika klabu hiyo maarufu duniani.

Baada ya kuondoka Real Madrid mwaka 2022, Marcelo alijiunga kwa muda mfupi na Olympiacos ya Ugiriki, kisha akarudi Fluminense kwa msimu wake wa mwisho 

Mechi yake ya mwisho rasmi ilichezwa Oktoba 26, 2024, dhidi ya EC Vitória katika ligi ya Brazil.

Marcelo anahesabiwa kama mmoja wa mabeki wa kushoto bora zaidi kuwahi kucheza mchezo wa soka.

Alijulikana kwa kasi yake, uwezo wa kudhibiti mpira, mashambulizi makali kutoka pembeni, na ubunifu mkubwa uwanjani.

Katika timu ya taifa ya Brazil, alicheza jumla ya mechi 58, akiwakilisha taifa lake katika michuano mbalimbali, ikiwemo Kombe la Dunia.

Katika maisha yake ya soka, Marcelo ametwaa mataji 28 ya kimataifa, 25 kati ya hayo akiwa na Real Madrid. Kwa mchango wake mkubwa katika klabu hiyo, alitajwa kama mmoja wa viongozi wa kihistoria wa Madrid na hata kuvaa beji ya unahodha wa timu.

 Licha ya kuhitimisha safari yake kama mchezaji, Marcelo amesisitiza kuwa bado ana ndoto na mipango mikubwa katika soka. Ingawa hajaweka wazi atajihusisha vipi na mchezo huo, mashabiki wake wanatarajia kumuona akiendelea kutoa mchango mkubwa kwa kizazi kipya cha wanasoka.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved