
Mshambuliaji wa zamani wa Manchester City, Sergio Agüero, anajikuta katika hali ya utata baada ya ahadi yake tata kabla ya mechi ya Ligi ya Mabingwa kati ya Manchester City na Real Madrid.
Kabla ya mchuano huo uliofanyika kwenye uga wa Etihad, Agüero alitoa kauli yenye utata akisema, "Ikiwa Real Madrid itashinda, nitakata tezi ndume zangu."
Maneno haya, ambayo yalionekana kama mzaha wa kuonesha imani yake kwa City, sasa yamegeuka mzigo mzito baada ya Real Madrid kuibuka na ushindi wa 2-3.
Katika mechi hiyo ya mchujo ya Ligi ya Mabingwa, Manchester City walijikuta wakizidiwa nguvu na Los Blancos, huku magoli ya Kylian Mbappe, Brahima Diaz na Jude Bellingham yakiwapa ushindi wenye thamani kubwa.
Hali hii imesababisha mashabiki wa soka, hususan wale wa Real Madrid, kumbana Agüero kuhusu ahadi yake isiyo ya kawaida.
Baada ya kipenga cha mwisho kulia, mitandao ya kijamii ilifurika jumbe kutoka kwa mashabiki waliomkumbusha Agüero juu ya ahadi yake. Wengine walienda mbali zaidi na kuunda vibonzo vya kejeli, wakimuuliza lini anapanga kutimiza maneno yake.
Agüero, ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa soka na mtangazaji wa mitandaoni, bado hajatoa tamko rasmi kuhusu ahadi hiyo, lakini amekuwa akichukulia mzaha shinikizo linaloendelea.
Hata hivyo, mashabiki wengi wanaelewa kuwa kauli yake ilikuwa tu njia ya kusisitiza uaminifu wake kwa Manchester City na hakuwa na nia ya kweli ya kutekeleza alichosema.
Hii si mara ya kwanza kwa mchezaji kutoa ahadi yenye utata kabla ya mechi kubwa. Wachezaji na wachambuzi wa soka mara nyingi hutabiri matokeo kwa njia ya mzaha, lakini kauli ya Agüero imevutia hisia kali kutokana na uzito wake.
Wakati City wakijizatiti kwa mechi ya marudiano kwenye dimba la Santiago Bernabue, itabakia kusubiriwa kuona kama Agüero ataibuka na kauli mpya au ataendelea kuzungusha mashabiki kwa majibu ya kejeli.
Je, unadhani Agüero anapaswa kutimiza ahadi yake, au ilikuwa tu mzaha wa kimichezo? Tuambie maoni yako!