
Klabu ya Soka ya Arsenal imeandika historia mpya katika Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuichapa PSV Eindhoven 7-1 ugenini katika hatua ya 16 bora.
Ushindi huu wa kishindo, uliopatikana Jumatatu, Machi 4, 2025, si tu umeweka rekodi mpya kwa klabu hiyo, bali pia umeingia kwenye historia ya michuano ya Ligi ya Mabingwa.
Matokeo haya yameipatia Arsenal ushindi wake mkubwa zaidi wa ugenini katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Ulaya, wakivunja rekodi ya ushindi wa 5-1 dhidi ya Inter Milan mwaka 2003 na dhidi ya Sporting CP mnamo Novemba 2024.
Katika historia ya michuano yote ya Ulaya, ushindi huu wa 7-1 dhidi ya PSV unashikilia nafasi ya tatu kwa ushindi mkubwa wa ugenini wa Arsenal, nyuma ya ushindi wa 7-0 dhidi ya Standard Liege mwaka 1993 kwenye Kombe la Washindi wa UEFA na ushindi wa 7-1 dhidi ya Copenhagen XI mwaka 1963.
Kwa ushindi huu, Arsenal imekuwa timu ya kwanza katika historia ya Ligi ya Mabingwa kufunga mabao saba ugenini katika hatua ya mwondoano.
Pia, walifunga mabao matano ndani ya dakika 48 za kwanza, jambo ambalo hakuna timu nyingine iliyowahi kufanya katika hatua hii ya mashindano.
Kwa PSV, ilikuwa usiku wa kukumbukwa kwa njia mbaya kwani ilikuwa mara yao ya kwanza kuruhusu zaidi ya mabao matano katika mechi ya nyumbani kwenye mashindano ya Ulaya.
Huu ulikuwa ushindi wa kwanza wa Arsenal kwenye ardhi ya Uholanzi tangu mwaka 2008 walipoifunga Twente. Pia, ilikuwa mara ya kwanza kwa Arsenal kufunga zaidi ya mabao matatu katika mechi ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa.
Kwa mara ya pili katika historia yao ya Ligi ya Mabingwa, Arsenal walifunga mabao saba kwenye mechi moja, mara ya kwanza ikiwa ni dhidi ya Slavia Prague mwaka 2007 kwenye Uwanja wa Emirates.
Mchezaji kinda Ethan Nwaneri aliweka rekodi kwa kuwa mchezaji wa tatu mdogo zaidi kufunga bao katika hatua ya mwondoano ya Ligi ya Mabingwa, nyuma ya Bojan (2008) na Jude Bellingham (2021).
Pia, Arsenal ilianza mechi na wachezaji wawili wa umri mdogo, Nwaneri na Myles Lewis-Skelly, kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2014 dhidi ya Galatasaray.
Kwa ushindi huu wa
kihistoria, Arsenal sasa imejihakikishia nafasi nzuri kuelekea mechi ya
marudiano na imeongeza matumaini yao ya kufika hatua za juu za michuano hii kwa
mara ya kwanza tangu walipofika fainali mwaka 2006