Ulimwengu wa soka umegubikwa na majonzi kufuatia kifo cha Joe Thompson, kiungo wa zamani aliyewahi kupitia akademia ya Manchester United, aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 36 baada ya kupambana na saratani kwa mara ya tatu.
Thompson, aliyezaliwa Bath na kulelewa Rochdale, aligunduliwa na saratani ya lymphoma ya kiwango cha nne mwaka jana, aina ya saratani ya damu iliyokuwa imeenea hadi kwenye mapafu. Ingawa alishinda ugonjwa huo mara mbili wakati wa uchezaji wake, safari yake ya mwisho dhidi ya maradhi hayo haikufua dafu.
Marehemu aliwahi kujiunga na Manchester United akiwa na miaka tisa kabla ya kujiunga na Rochdale, ambako alicheza kwa muda mrefu katika kipindi chake cha miaka 13 ya uchezaji. Alistaafu rasmi soka mwaka 2019.
Klabu ya Rochdale ilithibitisha kifo chake kupitia taarifa rasmi ikisema: “Joe, aliyekuwa akipambana kwa ujasiri na saratani kwa mara ya tatu, amefariki dunia kwa amani akiwa nyumbani na familia yake siku ya Alhamisi.”
Waliongeza: “Kwa wale waliomfahamu kwa karibu, Joe — au ‘Joey T’ kama alivyokuwa anajulikana — alikuwa zaidi ya mchezaji. Alikuwa mume mpendwa kwa Chantelle na baba wa watoto wawili, Thailula na Athena Rae.”
Manchester United pia ilitoa salamu za rambirambi kwa nyota wao wa zamani wa akademia: “Alikuwa mfano wa maadili ya klabu yetu. Tunahuzunika sana kumpoteza Joe Thompson. Alikuwa mtu mwenye haiba ya kipekee na aliyekuwa na uhusiano wa kina na klabu tangu akiwa mdogo.”
Thompson aliweka historia mwaka 2018 alipoifungia Rochdale bao muhimu dhidi ya Charlton Athletic, bao lililosaidia klabu hiyo kubaki katika Ligi ya Daraja la Kwanza.
Baada ya kustaafu, alijikita katika shughuli za uhamasishaji na ushauri wa umma. Katika mahojiano na BBC mwaka jana, alisema: "Ingawa ni maumivu makubwa, nipo tayari kupambana tena. Nataka kuacha athari chanya kwa maisha ya watu wengi iwezekanavyo."
Klabu ya Rochdale imepanga kumuenzi kwa kuvaa vibandiko vyeusi katika mechi zao na kufanya heshima maalum katika mchezo ujao wa nyumbani.
“Urithi wa Joe utaishi milele – ni mmoja wetu,” ilihitimisha taarifa ya klabu hiyo.