MICHUANO YA EURO 2020

EURO 2020: Mount na Chilwell watengwa na kikosi cha Uingereza

Wawili hao walitangamana na mchezaji Billy Gilmour wa Uskoti ambaye alipatikana kuwa na virusi vya Korona.

Muhtasari

•Kulingana na ujumbe uliotolewa na timu ya Three Lions, wawili hao wametengwa kama tahadhari baada  ya mashauriano na kitengo cha afya ya umma Uingereza.

•Gilmour ambaye alichezea Uskoti mechi kamili yake ya kwanza Ijumaa lipimwa kuwa na maradhi ya COVID 19 siku ya Jumapili na atajitenga kwa kipindi cha siku kumi.

Ben Cilwell, Billy Gilmour na Mason Mount katika mechi ya Uingereza dhidi ya Uskoti Ijumaa
Ben Cilwell, Billy Gilmour na Mason Mount katika mechi ya Uingereza dhidi ya Uskoti Ijumaa
Image: Hisani

Wachezaji wawili wa timu ya taifa ya Uingereza almaarufu kama 'Three Lion' wametengwa kufuatia kutangamana na mchezaji Billy Gilmour wa Uskoti ambaye alipatikana kuwa na virusi vya Korona.

Ben Chilwell na Mason Mount ambao wanachezea klabu ya Chelsea wanadaiwa kutangamana na  mwenzao Gilmour kwenye mechi kati ya Uingereza na Uskoti usiku wa Ijumaa. Mechi hiyo iliisha sare tasa.

Kulingana na ujumbe uliotolewa na timu ya Three Lions, wawili hao wametengwa kama tahadhari baada  ya mashauriano na kitengo cha afya ya umma Uingereza.

Gilmour ambaye alichezea Uskoti mechi kamili yake ya kwanza Ijumaa lipimwa kuwa na maradhi ya COVID 19 siku ya Jumapili na atajitenga kwa kipindi cha siku kumi.

 Mount na Chilwell hawatatangamana na kikosi hicho kingine wakisubiria maamuzi ya afya ya umma. 

Wawili hao watakosa mechi dhidi ya Ucheki usiku wa leo.