Manchester United na Real Madrid zakubaliana kuhusu uhamisho wa Varane

Mchezaji huyo ameigharimu United pauni 42.5M na atatia saini mkataba wa miaka mitano baada ya kakamilisha kipindi cha karantini

Muhtasari

•United ilitangaza mafanikio ya kumpata mlinzi huyo wa kati raia wa Ufaransa kupitia tovuti rasmi ya klabu.

•Varane, 28, amekuwa katika klabu ya Madrid kwa kipindi cha takriban miaka kumi baada ya kusajiliwa kutoka klabu ya Lens mwaka wa 2011.

Image: HISANI

Klabu ya Manchester United imefikia makubaliano ya kumsajili mlinzi Raphael Varane kutoka Real Madrid.

United ilitangaza mafanikio ya kumpata mlinzi huyo wa kati raia wa Ufaransa kupitia tovuti rasmi ya klabu.

"ManchesterUnited ina furaha kutangaza kuwa klabu imeafikiana na Real Madrid kuhusu uhamisho wa mlinzi wa timu ya taifa ya Ufaransa na mshindi wa World Cup Raphael Varane. Vipimo vya kidaktari na makubaliano na mchezaji yatakamilishwa" United ilitangaza.

Varane, 28, amekuwa katika klabu ya Madrid kwa kipindi cha takriban miaka kumi baada ya kusajiliwa kutoka klabu ya Lens mwaka wa 2011.

Amehusishwa mara kwa mara kwenye timu ya taifa ya Ufaransa na alikuwa kwenye  kikosi kilichotwaa ushindi wa Kombe la Dunia mwaka wa 2018. Pia alihusishwa kwenye michuano ya EURO 2020 ambayo ilichezwa mwezi uliopita.

Mchezaji huyo ameigharimu United pauni 42.5M na atatia saini mkataba wa miaka mitano baada ya kakamilisha kipindi cha karantini.

Kwingineko mlinzi wa Tottenham Toby Alderweireld amejiunga na klabu ya Al-Duhail SC nchini Qatar baada ya maafikiano kupatikana kati ya klabu hizo mbili.

Mshambulizi wa Harambee Stars Michael Olunga alikuwa kwenye mstari wa mbele kumkaribisha mlinzi huyo kwenye klabu yake ya Al-Duhail.