Messi azinduliwa rasmi kama mchezaji wa PSG

Messi ambaye ana umri wa miaka 34 atavalia jezi nambari 30

Muhtasari

•PSG ilitangaza usajili wa Messi kupitia kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii jioni ya Jumanne.

•Neymar ambaye aliwahi kucheza na Messi wakiwa Barcelona alionekana kujawa na bashasha na kupakia picha yao wakiwa pamoja enzi zile na kuandika ujumbe mfupi maalum "Pamoja tena"

•Uhusiano wake na Barcelona ulitamatika wiki iliyopita baada ya klabu hiyo kushindwa kumpatia mkataba mpya kufuatia matatizo ya kifedha. 

Image: TWITTER// PSG_INSIDE

Hatimaye staa wa soka Lionel Messi amezinduliwa rasmi kama mchezaji wa klabu ya PSG.

Mshambulizi huyo kutoka Argentina ametia saini kandarasi ya miaka miwili na mabingwa mara tisa wa Ligue 1.

PSG ilitangaza usajili wa Messi kupitia kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii Jumanne jioni.

"Paris Saint-Germain inafurahia kutangaza usajili wa Leo Messi kwa kandarasi ya miaka miwili na uwezekano wa mwaka wa tatu" PSG iliandika.

Messi ambaye ana umri wa miaka 34 atavalia jezi nambari 30 tofauti na nambari yake ya kawaida (10) aliyokuwa anavalia Barcelona na akichezea timu ya taifa.

Mshindi huyo wa tuzo la Ballon d'Or mara sita anaungana na washambulizi wengine matata duniani kama Neymar, Kylian Mbappe na Angel Di Maria.

Neymar ambaye aliwahi kucheza na Messi wakiwa Barcelona alionekana kujawa na bashasha na kupakia picha yao wakiwa pamoja enzi zile na kuandika ujumbe mfupi maalum "Pamoja tena"

Inaripotiwa kuwa Neymar alihusika sana katika uhamisho ule kwani alisaidia kumshawishi nyota huyo kukubali kujiunga na PSG.

Usajili wa Messi unaipatia klabu ya PSG nafasi bora kombe la ligi ya mabingwa bara Ulaya (Champions League) msimu ujao.

Messi ambaye ameichezea Barcelona kwa kipindi cha miaka 21 ameorodheshwa kama mmoja wa wachezaji bora zaidi wa wakati wote almaarufu kama 'G.O.A.T'.

Uhusiano wake na Barcelona ulitamatika wiki iliyopita baada ya klabu hiyo kushindwa kumpatia mkataba mpya kufuatia matatizo ya kifedha. 

Aliifungia Barcelona mabao 682 na kuibuka kama mfungaji bora wa  klabu hiyo tangu jadi.