Chelsea yanyakua taji la UEFA Super Cup baada ya kuzima Villareal kwenye penalti

Chelsea ilicharaza Villareal ya Uhispania 6-5 katika mikwaju ya penalti na kujinyakulia kombe la UEFA SUPER CUP usiku wa Jumatano.

Muhtasari

•Chelsea ilicharaza Villareal ya Uhispania 6-5 katika mikwaju ya penalti na kujinyakulia kombe la UEFA SUPER CUP usiku wa Jumatano.

•Mlinda lango wa Chelsea Kepa Arrizabalaga aliibuka bingwa wa mechi baada ya kuokoa penalti mbili za Villareal na kufanikisha klabu yake kutangazwa washindi wa kombe la Super Cup.

Image: TWITTER//CHELSEA

Meneja wa Chelsea Thomas Tuchel ameendelea kuonyesha umahiri wake huku akiongoza timu yake kunyakua kombe la pili tangu kuwasili kwake takriban miezi sita iliyopita.

Chelsea ilicharaza Villareal ya Uhispania 6-5 katika mikwaju ya penalti na kujinyakulia kombe la UEFA SUPER CUP usiku wa Jumatano.

Dakika 90 za kawaida na 30 za maongezi zilitamatika mechi hiyo ikiwa sare ya 1-1 na  kumaanisha kwamba mikwaju ya penalti ingeamua mshindi wa mchuano huo.

Bao la kipekee la Chelsea katika dakika za kawaida lilikuwa limefungwa na Hakim Ziyech katika dakika ya 27 huku bao la Villareal likifungwa na mshambulizi Gerard Moreno katika dakika ya  73.

Mlinda lango wa Chelsea Kepa Arrizabalaga aliibuka bingwa wa mechi baada ya kuokoa penalti mbili za Villareal na kufanikisha klabu yake kutangazwa washindi wa kombe la Super Cup.

Kepa aliokoa penalti ya mlinzi Aissa Mandi na Raul Albiol huku mlinda lango Sergio Asenjo wa Villareal akiokoa penalti moja tu ya mshambulizi Kai Havertz.

Kombe la UEFA Super Cup huwaniwa na mshindi wa ligi ya mabingwa Ulaya ( Champions League) na mshindi wa ligi ya Europa. Msimu uliopita, Chelsea  ilinyakua kombe la Champions League baada ya kupata ushindi dhidi ya Manchester City kwenye fainali ilhali Villareal ilishinda Manchester United katika fainali ya Europa League.