Rasmi! Manchester United yakamilisha usajili wa mshambulizi matata duniani Christiano Ronaldo

United imetangaza kuwa Ronaldo ametia saini mkataba wa miaka miwili na uwezekano wa nyongeza ya mwaka mwingine mmoja.

Muhtasari

•Mshindi huyo wa tuzo la Ballon D'Or mara tano amerejea Old Trafford baada ya takriban miaka 12 alipoondoka kujiunga na Real Madrid ya Uhispania.

•Ronaldo amesema kuwa anafurahia sana  hatua ya kurejea United kwani amekuwa akiithamini sana klabu hiyo moyoni.

Image: MANCHESTER UNITED

Klabu ya Manchester United imetangaza kukamilishwa kwa uhamisho wa nyota wa soka duniani Christiano Ronaldo kutoka Juventus.

Kupitia tovuti rasmi ya klabu, United imetangaza kuwa Ronaldo ametia saini mkataba wa miaka miwili na uwezekano wa nyongeza ya mwaka mwingine mmoja.

Mshindi huyo wa tuzo la Ballon D'Or mara tano amerejea Old Trafford baada ya takriban miaka 12 alipoondoka kujiunga na Real Madrid ya Uhispania.

Ronaldo amesema kuwa anafurahia sana  hatua ya kurejea United kwani amekuwa akiithamini sana klabu hiyo moyoni. 

"Manchester United ni klabu ambayo nimekuwa nikiithamini sana moyoni na nimefurahishwa na jumbe anbazo nimepokea tangu tangazo litolewe siku ya Ijumaa. Siwezi kusubiri kucheza ugani Old Trafford mbele ya mashabiki wengi. Natazamia sana kuungana na timu baada ya kipindi cha mapumziko na natumai tutakuwa na msimu wa kufana." Ronaldo amesema.

Kwa upande wake meneja wa United Ole Gunnar Solskjaer amemsifia sana Ronaldo kama mtu spesheli na kusema kuwa ana matumaini makubwa kuwa uzoefu wake utakuwa muhimu sana kwa wachezaji wadogo ambao wako kwenye kikosi.

"Yeye sio mchezaji bora tu ila pia binadamu maalum. Jambo la kuwa  na nia na uwezo wa kucheza katika hali ya juu kwa kipindi kirefu linahitaji mtu spesheli. Sina shaka kuwa ataendelea kutufurahisha na uzoefu wake utakuwa muhimu kwa kikosi chetu kidogo" Solskjaer amesema.

Mashabiki pamoja na wachezaji wa United wa sasa na wa hapo awali wamemkaribisha staa huyo  na kueleza hamu yao kubwa ya kumwona tena ugani Old Trafford.