"Tupatane nje ya uwanja" Mshambulizi Allan Wanga atangaza kustaafu kwake baada kucheza soka miaka 14

Muhtasari

•Wanga 35, ambaye ameshirikishwa kwenye timu ya Harambee Stars kutoka mwaka wa 2007 alitangaza kustaafu kwake kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.

•Wanga amechezea klabu nyingi nchini ikiwemo Lolwe FC, Sher Karuturi, Tusker, AFC Leopards na Kakamega Homeboyz. Kimataifa Wanga amechezea Petro Atletico ya Angola, FC Baku ya Azerbaijani, Al- Merrikh ya Sudan, Hoang Anh Gia Lai ya Vietnam na Azam ya Tanzania.

Image: FACEBOOK// ALLAN WANGA

Mshambulizi matata wa timu ya taifa na klabu ya Kakamega Homeboyz Allan Wetende Wanga ametangaza kustaafu kwake baada ya kucheza soka ya kitaalamu kwa kipindi cha miaka 14.

Wanga 35, ambaye ameshirikishwa kwenye timu ya Harambee Stars kutoka mwaka wa 2007 alitangaza kustaafu kwake kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Mchezaji huyo amesema kuwa soka imempeleka mahali kwingi duniani ambako hakuwahi fikiria angewahi kufika.

Amesema kwamba amefurahia kipindi cha miaka 14 ambacho amekuwa akichezea timu ya taifa na klabu mbalimbali na kuwashukuru sana mashabiki ambao wamekuwa wakimtia motisha wa kucheza vyema zaidi.

"Miaka 14 nikifanya kitu ambacho kinakuleta raha, kuridhika na fahari  ni baraka. Nimekuwa nikiishi kwa hii baraka tangu nicheze kandanda kwa mara ya kwanza nikiwa mtoto mdogo na nikaanza kucheza soka ya kitaalam.

Mapenzi yangu kwa soka imenipeleka mahali ambako sikuwahi dhania ningewahi fika nikiwa na timu ya taifa na klabu. Nimeshuhudia ushindi na kupoteza, nimeinua vikombe, nimevumilia uchungu wa kukosa ushindi licha ya kuwa karibu nao, nimepitia yote.

Nimekuwa nikipewa msukumo na mapenzi pamoja na kuungwa mkono na mashabiki. Bila nyinyi mashabiki, wachezaji wenzangu, familia na wasaidizi katika klabu zote ambazo nimechezea singekuwa na motisha wa kuendelea mbele.Tafadhali pokeeni shukran zangu kwa yote, mliniinua wakati nilihitaji kuboresha mchezo wangu.

Ninapostaafu ningependa kuchukua fursa hii kuwapa shukran zangu. Nilikuwa hapo kwa kuwa mlikuwa na mimi. Shukran na Mungu awabariki. Tupatane nje ya uwanja." Wanga aliandika kwenye ukurasa wake wa Faceboook.

Wanga amechezea klabu nyingi nchini ikiwemo Lolwe FC, Sher Karuturi, Tusker, AFC Leopards na Kakamega Homeboyz. Kimataifa Wanga amechezea Petro Atletico ya Angola, FC Baku ya Azerbaijani, Al- Merrikh ya Sudan, Hoang Anh Gia Lai ya Vietnam na Azam ya Tanzania.