Matokeo ya wiki ya 5 ya EPL 2021/22, Hali ilivyo kwenye jedwali

Muhtasari

•Wanabunduki walipata ushindi wao wa pili msimu huu baada ya kulemea wenyeji wao Burnley. Bao la pekee la mechi hiyo lilifungwa na kiungo Martin Odegaard katika dakika ya 30.

•Tottenham walishindwa kulenga lango la wageni wao huko Thiago Silva, Ngolo Kante na Antonio Rudiger wakipatia Chelsea ushindi wa 0-3 na kuwapeleka kileleni mwa jedwali.

Image: TWITTER// CHELSEA

Wiki ya tano ya michuano ya EPL 2021/22 ilishuhudia mechi kumi za kusisimua huku jedwali likiendelea kuchukua sura.

Mechi ya kwanza ilichezwa usiku wa Ijumaa ambako Newcastle walitoka sare ya 1-1 na wageni wao Leeds United.

Michuano sita ilichezwa siku  ya Jumamosi, mechi ya kwanza ikiwa katia ya Wolves na Brentford ambapo Brentford waliapata ushindi wa mabao mawili bila jawabu licha ya kupunguzwa hadi wachezaji 10 baada ya kiungo Shandon Baptiste kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 64.

Klabu nane ziliingia viwanjani mida ya saa kumi na moja siku ya Jumamosi.

Wanabunduki walipata ushindi wao wa pili msimu huu baada ya kulemea wenyeji wao Burnley. Bao la pekee la mechi hiyo lilifungwa na kiungo Martin Odegaard katika dakika ya 30.

Liverpool walipata ushindi mkubwa wa 3-0 dhidi ya wageni wake Crystal Palace. Mo Salah, Sadio Mane na Naby Keita walifungia mabingwa hao wa EPL 2019 bao moja kila mmoja wao.

Mabingwa wa Ligi Kuu msimu uliopita Manchester City walishindwa kuwafunga wageni wao Southampton na mechi ikaishia sare ya 0-0.

Watford walipata ushindi wa 3-1 ugenini dhidi ya Norwich City. Emmanuel Dennis (1) na Ismaila Sarr (2) walifungia Watford huku Teemu Pukki akifungia Norwich bao lake la pekee.

Aston Villa walipata ushindi mkubwa wa 3-0 dhidi ya wageni wake Everton. Kiungo Matty Cash, mshambulizi Leon Bailey walifungia Villa bao moja moja huku beki Lucas Digne akijifunga bao moja.

Mechi tatu kubwa pekee zilichezwa siku ya Jumapili.

Brighton walipata ushindi wa kushangaza wa 2-1 dhidi ya mabingwa wa EPL 2015/2016 Leicester City. Neal Maupay na Danny Welbeck walifungia wenyeji huku Leicester wakifungiwa na Jamie Vardy.

Manchester United waliweza kunyakua pointi tatu katika dakika za mwisho wakicheza na West Ham ugani Olympic. LIngard aliingia na kufunga katika dakika ya 89 na kuwapatia Mashetani Wekundu ushindi wa 2-1. Christiano Ronaldo alikuwa amefungia United bao la kwanza katika dakika ya 35 huku bao la pekee la West Ham likifungwa na  Said Benrahma.

Mechi kubwa ya wikendi ilikuwa kati ya miamba wawili wa jiji la London Tottenham Hotspurs na Chelsea ambao walimenyana  mida ya saa kumi na mbili unusu.

Tottenham walishindwa kulenga lango la wageni wao huko Thiago Silva, Ngolo Kante na Antonio Rudiger wakipatia Chelsea ushindi wa 0-3 na kuwapeleka kileleni mwa jedwali.

Kwa sasa Chelsea, Liverpool na Manchester United wanashikilia nafasi za 1,2,3 mtawalia wakiwa na pointi 13 kila mmoja huku Newscastle, Burnley na Norwich wakishikilia nafasi za mwisho tatu na pointi 2, 1, 0 mtawalia.