'Nitakuwa tayari wakati mwingine" Bruno Fernandes ajitetea baada ya kukosa penalti katika dakika za ziada

Muhtasari

•Vijana wa Ole Gunnar Solskjaer walikuwa na matumaini ya kuzoa alama moja angalau katika dakika za mwisho mwisho baada ya refa Mike Dean kuwatunuku penalti ila ndoto hizo zikafifia baada ya kiungo mahiri Bruno Fernandes kutia nguvu nyingi kwenye mpira na kuupiga juu ya goli.

•Alisema kwamba licha ya kukosa kufunga penalti aliyopewa jukumu la kupiga katika dakika za ziada, bado ataendelea kuchukua jukumu hilo kila anapopatiwa.

Image: HISANI

Jumamosi, Septemba 25 si miongoni mwa siku ambazo mashabiki pamoja na wachezaji wa Manchester United wangependa kukumbuka maishani mwao.

Miamba hao wa soka kutoka jijini Manchester walishindwa kuenda kileleni mwa jedwali baada ya kupokea kichapo cha 0-1 nyumbani wakicheza dhidi ya Aston Villa.

Vijana wa Ole Gunnar Solskjaer walikuwa na matumaini ya kuzoa alama moja angalau katika dakika za mwisho mwisho baada ya refa Mike Dean kuwatunuku penalti ila ndoto hizo zikafifia baada ya kiungo mahiri Bruno Fernandes kutia nguvu nyingi kwenye mpira na kuupiga juu ya goli.

Baada ya kushindwa kupatia timu yake alama moja ya kufuta machozi, Bruno alitumia kurasa zake za mitandao kujitetea na kuwashukuru mashabiki waliomuunga mkono na kumpa motisha licha ya kilichotokea uwanjani.

"Hakuna aliyefadhaika zaidi yangu kwa kukosa kufunga penalti na kupoteza mechi ya leo. Nimekuwa nikichukua majukumu yangu na kuyakumbatia chini ya shinikizo katika nyakati kama hizi. Leo nilishindwa. 

Lakini nilichukua jukumu hilo na tamaa na uwajibikaji kama tu nyakati ambazo nimewahi kufunga." Bruno alisema.

Staa huyo raia wa Ureno amesema kwamba amezoea kukosolewa na huwa anatumia nafasi kama ile kujiboresha .

"Kukosolewa na maono tofauti ni sehemu ya mpira. Nimejifunza kuishi na kwenyewe na hata kutumia fursa hiyo kujipatia msukumo wa kuwa mchezaji bora" Alisema Bruno.

Alisema kwamba licha ya kukosa kufunga penalti aliyopewa jukumu la kupiga katika dakika za ziada, bado ataendelea kuchukua jukumu hilo kila anapopatiwa.

"Jambo muhimu kwangu ni kupata ushindi pamoja na nitafanya chochote niwezacho kusaidia wenzangu na klabu kuwa bora zaidi.  Shukran kwa kusimama nami baada ya kipenga kupulizwa. Kuskia jina langu likiimbwa uwanjani lilikuwa tendo la kihisia. Nitarejea nikiwa bora zaidi kwangu binafsi na kwa wenzangu na mashabiki ambao wameishi kunishikilia" Bruno alisema.

Kwa sasa United inashikilia nafasi ya nne na alama 13 baada ya kucheza mechi sita.