Wiki ya pili ya mashindano ya ligi ya mabingwa (Champions League) ilitamatika usiku wa Jumatano huku mechi nane zikichezwa.
Mechi hizo zilihusisha klabu 16 zilizo kwenye kundi E, F, G na H.
Mechi mbili za kwanza zilichezwa mwendo wa saa mbili kasorobo ambapo Atlanta walipiga Young Boys 1-0 nyumbani huku Zenit St Petersburg wakipata ushindi mkubwa wa 4-0 dhidi ya Malmo FF ambayo ililazimika kukamilisha mechi na wachezaji 10 baada ya beki Anel Ahmedhodzic kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 53.
Mechi zingine sita zilichezwa mida ya saa nne ambapo Juventus waliwazima washindi wa kombe hilo msimu uliopita Chelsea kwa kuwapiga 1-0 nyumbani huku Barcelona wakiumizwa ugenini kwa mabao 3 bila jawabu.
Mashetani wekundu walilipiza kisasi kwa Villareal kwa kuwacharaza 2-1 ugani Old Trafford miezi minne tu baada ya vijana hao wa Unai Emery kuwazuia kunyakua kombe la Europa msimu uliopita. Mabao ya United yalifungwa na beki Alex Telles na mshambulizi matata Christiano Ronaldo.
Miamba wa soka nchini Ujerumani Bayern Munich walipata ushindi mkubwa wa 5-0 dhidi ya Dynamo Kyiv ya Ukrania huku Salzburg wakishinda 2-1 nyumbani dhidi ya Lille.
Mechi kati ya Wolfsburg na Sevilla iliisha sare ya 1-1 licha ya wenyeji kupata kadi nyekundu katika dakika ya 85.
Kwa sasa PSG inaongoza kundi A, Liverpool kundi B,Ajax wako kileleni katika kundi C, Sherrif Tiraspol hawajabanduliwa katika kundi D, Bayern inatawala kundi E, Atlanta kundi F, Salzburg wako kileleni katika kundi G huku Juventus wakiongoza kundi H.