Tamko la Mbappe kumuita Neymar 'makalio' lazua hisia

Muhtasari

•Kiungo huyo wa miaka 22 alisikika akisema ''huyu makalio, hawezi kunipigia pasi'' baaada ya kutolewa uwanjani wakati wa mechi yao dhidi ya Montpellier.

Mbappe (kushoto) amefunga mabao 136 katika mechi 182 za PSG tangu alipowasili kutoka Monaco Augosti 2017
Mbappe (kushoto) amefunga mabao 136 katika mechi 182 za PSG tangu alipowasili kutoka Monaco Augosti 2017
Image: REUTERS

Kylian Mbappe anasema alizungumza na mchezaji mwenzake Neymar katika klabu ya Paris St-Germain kuhusiana na tamko la matusi alilotumia dhidi ya Mbrazil huyo katika mojawapo ya mechi zao mwezi uliopita.

Kiungo huyo wa miaka 22 alisikika akisema ''huyu makalio, hawezi kunipigia pasi'' baaada ya kutolewa uwanjani wakati wa mechi yao dhidi ya Montpellier.

"Ndio, ni kweli, Nilisema hivyo. Haya ni mambo hutokea kila wakati katika soka," alisema Mbappe ambaye pia ni mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ufaransa.

"Mara baada ya kugundua tamko hilo limegeuka kuwa kubwa, Nilisema naye."

PSG ilishinda 2-0 katika mechi ya Ligue 1 dhidi ya Montpellier kabla ya kuinyuka Manchester City mabao 2-0 katika mechi ya Ligi ya Mabingwa awamu ya makundi.

Akizungumza katika mahojiano na L'Equipe, Mbappe aliongeza: ''Tushawahi kujibizana manenu kama hayo siku zilizopita na tutaendelea kufanya hivyo, kwa sababu tunataka kushinda, lakini hatufanyi hivyo kwa nia mbaya"

Hakuna chuki kabisa kwa sababu namheshimu kama mchezaji na mwanamume , na pia napenda kile anachofanya."

Mbappe alikua ameambia RMC Sport wiki hii kwamba "aliomba kuondoka" PSG licha ya kunyatiwa na Real Madrid wakati wa kiangazi, akizungumza na L'Equipe, aliongeza kuwa tangu wakati huo hakuna mazungumzo yaliyofanyika kuhusu mkataba mpya baada ya msimu ujao.

"Nimekua katika soka kwa muda mrefu kiasi kutambua ukweli wa jana hauwezi kuwa wa leo, au hata kesho," alisema.

"Laiti ningeliambiwa kwamba [Lionel] Messi atachezea PSG, nisingeliamini, kwa hivyo huwezi kujua ni nini kinaweza kutokea."

Mbappe aliongeza: "Kwa sasa, kesho yangu sio muhimu. Nimepoteza nguvu nyingi msimu huu wa kiangazi, na ilichosha sana."