Masaibu ya Harambee Stars: Rais wa FKF Nick Mwendwa anyoshewa kidole cha lawama kwa matokeo hafifu

Muhtasari

•Uteuzi wa kocha Engin Firat mwezi uliopita uliizua gumzo kubwa mitandaoni wengi wakionekana kukosoa hatua hiyo.

•Baadhi ya wakenya walihoji jinsi  Mwendwa alivyoafikia uteuzi huo huku wakieleza wasiwasi wao kuhusiana na matokeo hafifu ambayo kocha Firat ameandikisha na timu ambazo amekuwa akisimamia hapo awali.

Image: MAKTABA

Timu ya taifa ya soka Harambee Stars haijapata ushindi wowote kwenye mechi tatu za kufuzu kwa kombe la dunia ambazo zimechezwa hivi karibuni.

Mechi iliyochezwa usiku wa Alhamisi kati ya Harambee Stars na Mali imeibua ghadhabu kubwa mitandaoni miongoni mwa mashabiki wa soka nchini ambao wameeleza kutoridhika kwao.

Harambee Stars walipoteza 5-0 dhidi ya wenyeji wao kwenye mechi yake ya tatu katika kundi E, matokeo ambayo yameacha wengi wakimnyooshea rais wa Shirikisho la soka nchini Nick Mwendwa kidole cha lawama.

Uteuzi wa kocha Engin Firat mwezi uliopita uliizua gumzo kubwa mitandaoni wengi wakionekana kukosoa hatua hiyo.

Baadhi ya wakenya walihoji jinsi  Mwendwa alivyoafikia uteuzi huo huku wakieleza wasiwasi wao kuhusiana na matokeo hafifu ambayo kocha Firat ameandikisha na timu ambazo amekuwa akisimamia hapo awali.

Takriban wiki tatu baadae wasiwasi kuhusiana na uamuzi huo umeongezeka baada ya ndoto za Harambee Stars za kushiriki katika kombe la dunia mwaka ujao kuangamizwa zaidi na Mali.

Baadhi ya wanamitandao wamehusisha  rais wa FKF Nick Mwendwa na  masaibu ambayo yamekumba Harambee Stars.

Kiongozi huyo aliangaziwa sana kwenye mtandao wa Twitter asubuhi ya Ijumaa huku baadhi ya wanamitandao wakimshinikiza ajiuzulu.

Je, maoni yako  ni yepi kuhusu masaibu ya Harambee Stars?