EPL 2021/22: Matokeo ya Jumamosi, ratiba ya Jumapili

Muhtasari

•Michuano ya raundi ya tisa iliendelea siku ya Jumamosi huku mechi sita za kusisimua zikichezwa katika nyanja mbalimbali nchini Uingereza.

•Chelsea walipata ushindi mkubwa zaidi kuwahi shuhudiwa msimu huu baada ya kuwalaza Norwich mabao 7 bila jawabu

•Mechi tatu zaidi zinatarajiwa kupigwa siku ya Jumapili huku mechi kati ya Manchester United na Liverpool iliyosubiriwa kwa hamu na ghamu ikichezwa mwendo wa saa kumi na mbili unusu ugani Old Trafford

Image: INSTAGRAM// CHELSEA

Raundi ya tisa ya mashindano ya EPL iling'oa nanga usiku wa Ijumaa huku mechi kati ya Arsenal na Aston Villa ikichezwa mida ya saa nne unusu usiku.

Wanabunduki waliweza kuonyesha makali yao kwa kuwapiga vijana wa Dean Smith 3-1 nyumbani licha ya kuandikisha matokeo hafifu  dhidi  yao msimu uliopita. Mabao ya Thomas Partey, Pierre-Emerick Aubameyang na Emile Smith Rowe yalipatia klabu hiyo ya London ushindi huku Jacob Ramsey akifungia Villa bao la kufutia machozi.

Michuano ya raundi ya tisa iliendelea siku ya Jumamosi huku mechi sita za kusisimua zikichezwa katika nyanja mbalimbali nchini Uingereza.

Mechi ya kusisimua zaidi na ambayo ilishuhudia mabao mengi kati ya Chelsea na Norwich ugani Stamford Bridge ilifungua ratiba ya Jumamosi.

Miamba hao wa soka kutoka London walipata ushindi mkubwa zaidi kuwahi shuhudiwa msimu huu baada ya kuwalaza Norwich mabao 7 bila jawabu. Hat-trick ya Mason Mount, bao la kujifunga la Max Aarons na mabao ya Calum Hudson-Odio, Recce James, Ben Chilwell yalipatia mabingwa hao wa Champions League ushindi.

Mechi nne zaidi zilichezwa mwendo wa saa kumi na moja jioni ambapo ushindi mmoja na sare tatu zilishuhudiwa.

Mechi kati ya Leeds na Wolves na ile ya Crystal Palce dhidi ya Newcastle ziliishia sare ya 1-1 huku mechi kati ya Southampton na Burnley ikiandikisha sare ya 2-2.

Mchuano kati ya Everton na Watford ulishuhudia mabao saba huku tano yakiwa ya wageni Watford huku wenyeji wakiweza kufunga mawili tu. Licha ya vijana wa Rafa Benitez kutangulia kufunga katika dakika ya tatu, Watford waliweza kuamka na kutia wavuni mabao matano ikiwemo hat-trick ya mshambulizi Joshua King.

Mechi ya mwisho siku ya Jumamosi ilikuwa kati ya Brighton na washindi wa EPL msimu uliopita Manchester City.

Vijana wa Guardiola waliweza kuwika ugenini  1-4 kupitia mabao ya Ikay Gundogan, Phil Foden (2) na Riyad Mahrez. Bao la pekee la Brighton lilifungwa na Mac Alister kupitia mkwaju wa penalti.

Mechi tatu zaidi zinatarajiwa kupigwa siku ya Jumapili huku mechi kati ya Manchester United na Liverpool iliyosubiriwa kwa hamu na ghamu ikichezwa mwendo wa saa kumi na mbili unusu ugani Old Trafford

Michuano miwili, Brentford dhidi ya Leicester na West Ham dhidi ya Tottenham itatangulia kuchezwa saa kumi alasiri..