Arsenal, Chelsea na Sunderland zatamba Carabao

Muhtasari

•Arsenal, Chelsea na Sunderland ziliweza kujihifadhia nafasi katika robo fainali baada ya kupata ushindi dhidi ya wapinzani wao.

•Michuano 5 zaidi itachezwa usiku wa Jumatano ambapo West Ham watakaribisha Manchester City, Leicester wakaribishe Brighton, Liverpool watakuwa wageni wa Preston, Tottenham watembelee Burnley huku Stoke City wakimenyana na Brentford nyumbani.

Image: INSTAGRAM// ARSENAL

Kombe la EFL Carabao liliingia  katika hatua ya kufuzu kuingia robo fainali usiku wa Jumanne huku jumla ya mechi tatu za kwanza zikichezwa mwendo wa saa nne kasorobo.

Arsenal, Chelsea na Sunderland ziliweza kujihifadhia nafasi katika robo fainali baada ya kupata ushindi dhidi ya wapinzani wao.

Wanabunduki waliweza kunyuka Leeds United mabao mawili bila jawabu katika kipindi cha pili na kunyakua pointi zote tatu. Mabao ya Arsenal yalifungwa na Calum Chambers pamoja na Eddie Nketiah.

The Blues waliweza kuwabandua nje wapinzani wao Southampton kupitia mikwaju ya penalti baada mechi kuishia sare ya 1-1 katika kipindi cha kawaida. Kai Havertz alifungia Chelsea katika kipindi cha kwanza huku Che Adams akisawazishia Southampton.

Vijana wa Thomas Tuchel waliweza kufunga penalti nne huku mikwaju mitatu pekee ya Southampton ikiweza kupenya langoni.

Mechi kati ya QPR na Sunderland iliishia sare tasa katika kipindi cha kawaida na kupeleka mechi katika mkondo wa penalti ambapo wageni Sunderland walifunga tatu huku wenyeji wakifunga moja tu.

Michuano 5 zaidi itachezwa usiku wa Jumatano ambapo West Ham watakaribisha Manchester City, Leicester wakaribishe Brighton, Liverpool watakuwa wageni wa Preston, Tottenham watembelee Burnley huku Stoke City wakimenyana na Brentford nyumbani.