logo

NOW ON AIR

Listen in Live

EPL 2021/22: Matokeo ya raundi ya 10, Hali ilivyo kwenye jedwali

Washambulizi Christiano Ronaldo,  Edinson Cavani na Marcus Rashford walisaidia mashetani wekundu kupata ushindi wa 3-0 dhidi ya Tottenham na kuongeza shinikizo dhidi ya kocha Nuno Espirito

image
na Radio Jambo

Burudani31 October 2021 - 16:12

Muhtasari


•Kwa sasa Chelsea inaongoza jedwali na pointi 25, Liverpool ya pili na pointi 22, Manchester City ya nne na pointi 20 huku West Ham ikifunga nne bora na pointi 20 pia.

Michuano ya kombe la EPL 2021/22 iliingia katika raundi ya 10 huku  jumla ya mechi tisa za kukata na shoka zikichezwa wikendi ambayo imetamatika.

Siku ya Jumamosi ilishuhudia michuano saba huku  mechi ya ufunguzi ikiwa kati ya washindi wa EPL 2015/16, Leicester City na wanabunduki ambayo ilichezwa mida ya saa nane unusu ugani King  Power.

Vijana wa Mikel Arteta waliendeleza fomu yao nzuri kwa kuwalaza vijana wa Brendan Rodgers mabao mawili bila jawabu. Beki Gabriel Magalhaes na kiungo mshambuliaji Emile Smith Rowe walisaidia wanabunduki kuwazima wapinzani wao katika kipindi cha kwanza.

Mechi tano zilichezwa mwendo wa saa kumi na moja huku nyingi zikiandikisha matokeo ya kushangaza mashabiki wa soka kote ulimwenguni.

Washindi wa EPL msimu uliopita walipoteza nyumbani dhidi ya Crystal Palace ambao waliwafunga mabao mawili kwa sufuri. Wilfred Zaha na Conor Gallagher ndio waliofungia Palace.

Liverpool walilazimika kugawana pointi na Brighton baada ya mechi iliyochezewa ugani Anfield kuishia sare ya 2-2. Jordan Henderon na Sadio Mane walifungia Liverpool huku Enock Mwepu na Leandro Trossard wakifungia Brighton.

Chelsea waliweza kubaki kubaki kileleni mwa jedwali baada ya kuwachapa wenyeji wao Newcastle mabao matatu bila jawabu na kunyakua pointi zote tatu.

Burnley waliwika nyumbani dhidi ya Brentford kwa kuandikisha ushindi wa 3-1 huku Southampton wakishinda 0-1 ugenini dhidi ya Watford.

Mechi kubwa ya wikendi ilikuwa kati ya Tottenham na Manchester United ambayo ilichezwa mwendo wa saa moja unusu. Washambulizi Christiano Ronaldo,  Edinson Cavani na Marcus Rashford walisaidia mashetani wekundu kupata ushindi wa 3-0 dhidi ya Tottenham na kuongeza shinikizo dhidi ya kocha Nuno Espirito.

Mechi mbili zilichezwa siku ya Jumapili, mechi ya ufunguzi ikiwa kati ya Norwich City na Leeds ambapo Leeds ilishinda 2-1 ugenini.

West Ham walipata ushindi mkubwa wa 4-1 ugenini dhidi ya Aston Villa na kuweza kuhifadhi nafasi ya nne kwenye jedwali. Benjamin Johnson, Declan Rice, Pablo Fornals na Jarrod Bowen walifungia The Hammers huku Ollie Watkins akifungia Villa bao la kufutia machozi.

Mechi ya mwisho ya raundi ya 20 kati yaWolves na Everton itachezwa mwendo wa saa tano usiku wa Jumatatu.

Kwa sasa Chelsea inaongoza jedwali na pointi 25, Liverpool ya pili na pointi 22, Manchester City ya nne na pointi 20 huku West Ham ikifunga nne bora na pointi 20 pia.

Nafasi tatu za mwisho zimekaliwa na Burnley, Newcastle na Norwich ambazo zimeandikisha pointi 7, 4 na 2 mtawalia.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved