Champions League 2021/22: Matokeo ya wiki hii, Hali ilivyo kwenye jedwali

Muhtasari

•Kwa sasa Manchester City inaongoza kundi A na pointi 9, Liverpool iko kileleni kundi B na pointi 12, Ajax inaongoza kundi C na pointi 12, Real Madrid kundi D na pointi 9,Bayern Munich kundi E na pointi 12, Manchester United imesonga kileleni kundi F na pointi 7, Salzburg yatawala kundi G na pointi 7 huku Juventus ikiongoza kundi H na pointi 12.

Robert Lewandoki
Robert Lewandoki
Image: HISANI

Wiki hii michuano ya ligi ya mabingwa Ulaya iliingia katika raundi ya nne kwenye hatua ya makundi huku mechi nane za kwanza zikichezwa siku ya Jumanne na zingine nane siku ya Jumatano.

Chelsea waliendeleza fomu yao nzuri huku wakichapa wenyeji wao usiku huo Malmo FF bao moja kwa bila. Hakim Ziyech ndiye aliyesaidia  The Blues kupata ushindi huo.

Wolfsburg waliweza kupata ushindi wa 2-1 nyumbani dhidi ya Salzburg mwendo wa saa tatu kasorobo.

Mechi sita zaidi zilichezwa mwendo wa saa tano usiku.

Bayern Munich waliendelea kuonyesha makali yao huku wakilaza wageni wao Benfica mabao matano kwa mawili. Robert Lewandoski alifunga hat-trick huku Leroy Sane na Serge Gnabry wakiongeza machungu moyoni mwa Benfica.

Mshambulizi matata Christiano Ronaldo alinusuru klabu yake ya Manchester United kutokana na aibu ya kichapo huku bao lake katika dakika ya 90+1 ikisaidia mashetani wekunde kusawazisha na kupata angalau pointi moja.  Mechi hiyo iliishia sare  ya 2-2.

Barcelona walishinda 1-0 kupitia mkwanju wa Ansu Fati ugenini dhidi ya Dynamo Kyiv huku Juventus wakishinda Zenit St Petersburg 4-2 nyumbani.

Villareal waliwika nyumbani dhidi ya Young Boys na kunyakua ushindi wa 2-0 huku Sevilla ikipoteza 1-2 nyumbani dhidi ya Lille.

Mechi za siku ya Jumatano ziling'oa nanga mwendo wa saa tatu kasorobo.

Miamba wa soka Uhispania Real Madrid walipata ushindi wa 2-1 nyumbani dhidi ya Shaktar Donetsk kupitia mabao ya Karim Benzema. Mechi kati ya AC Milan na FC Porto iliishia sare ya 1-1

Mechi sita zaidi zilichezwa mwendo wa saa tano usiku katika nyanja mbalimbali bara Ulaya.

Borrusia Dortmund ilipoteza 1-3 nyumbani dhidi ya Ajax baada ya beki Mats Hummels kuonyeshwa kadi nyekundu katik dakika ya 29.

Mabao ya Diogo Jota na Sadio Mane katika dakika 21 za kwanza yaliwezesha Liverpool kupata ushindi wa 2-0 dhidi ya Atletico Madrid ambayo beki wake Felipe alionyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 36.

Vijana wa Pep Guardiola walionyesha ubabe wao kwa kulaza wageni wao Club Brugge KV mabao manne kwa moja ugani Etihad.

Inter Milan waliwika ugenini dhidi ya Sheriff Tiraspol na kupata ushindi 3-1.

Mechi kati  ya RB Leipzig na PSG iliishia sare ya 2-2.

Sporting Lisbon ya Ureno ilipata ushindi mkubwa wa 4-1 dhidi ya Besiktas.

Kwa sasa Manchester City inaongoza kundi A na pointi 9, Liverpool iko kileleni kundi B na pointi 12, Ajax inaongoza kundi C na pointi 12, Real Madrid kundi D na pointi 9,Bayern Munich kundi E na pointi 12, Manchester United imesonga kileleni kundi F na pointi 7, Salzburg yatawala kundi G na pointi 7 huku Juventus ikiongoza kundi H na pointi 12.

Robert Lewandoski (8), Sebastian Haller (7), Christopher Nkunku (5), Christiano Ronaldo (5) na Mohammed Salah (5) wanaongoza kwa ufungaji wa mabao.