Norwich yamfuta kazi kocha Daniel Farke masaa machache baada ya kupata ushindi wa kwanza

Muhtasari

•Uamuzi wa kumtimua Farke uliafikiwa katika juhudi za kuboresha nafasi ya klabu hiyo kusalia katika EPL msimu huu utakapotamatika kuona kwamba imekuwa ikiandikisha matokeo duni tangu msimu ulipoanza.

Daniel Farke
Daniel Farke
Image: CANARIES.CO.UK

Klabu ya Norwich City imempiga kalamu kocha mkuu Daniel Farke.

Norwich ilitangaza kuondoka kwa Mjerumani huyo siku ya Jumamosi, masaa machache baada ya kuandikisha ushindi wa kwanza wa EPL msimu huu katika mechi dhidi ya Brentford.

Farke ambaye alisajiliwa mwaka wa 2017 amesimamia klabu hiyo katika mechi 208 huku akiiongoza kutwaa kombe la Championship mwaka wa 2017 na 2021.

Kulingana na taarifa ambayo ilichapishwa kwenye tovuti rasmi ya Norwich, uamuzi wa kumtimua Farke uliafikiwa katika juhudi za kuboresha nafasi ya klabu hiyo kusalia katika EPL msimu huu utakapotamatika kuona kwamba imekuwa ikiandikisha matokeo duni tangu msimu ulipoanza.

"Kila mtu hapa Norwich anafaa kushukuru Daniel na wasaidizi wake kwa sababu ya kazi kubwa ambayo amefanya katika safari yetu. Walitusaidia kupata mataji mawili, kumbukumbu nzuri na wakaleta katika falsafa yetu inavyomaanisha kuwa sehemu ya klabu hii ya kandanda" Mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo Stuart Webber alisema.

Farke anaiwacha Norwich ikiwa katika nafasi ya mwisho kwenye jedwali ya EPL baada ya kupoteza mechi 8, kuandikisha sare mbili na kushinda mechi moja pekee. 

Norwich ilipata ushindi wa kwanza msimu huu siku ya Jumamosi baada ya kupiga Brentford 1;2 ugenini.