Aston Villa yampiga kalamu kocha Dean Smith kufuatia msururu wa matokeo hafifu

Muhtasari

•Mkurugenzi mtendaji wa Villa Christian Purslow amesema uamuzi huo uliafikiwa sasa ili kupatia kocha mpya atakayeteuliwa wakati tosha wa kufanya mabadiliko ya kuboresha klabu.

•Villa imetangaza kwamba tayari wameanza juhudi za kusaka kocha atakayejaza nafasi iliyoachwa wazi na Smith.

Image: INSTAGRAM// DEAN SMITH

Klabu za soka za bara Ulaya zimeendelea kuwatimua kazi makocha ambao wameonekana kulemewa na kazi zao.

Klabu iliyofuta kocha wake hivi karibuni ni Aston Villa ambayo ilitangaza kuondoka kwa kocha Dean Smith siku ya Jumapili.

Smith ambaye ameongoza Villa tangu mwezi Oktoba mwaka wa 2018 alifutwa kazi baada ya klabu hiyo kupoteza katika mechi zote tano za hivi karibuni.

Mara ya mwisho Villa iliandikisha ushindi ilikuwa Septemba 25 ambapo ilishinda 0-1 ugenini dhidi ya Manchester United.

Mechi ya mwisho ambayo Smith alisimamia ilichezwa usiku wa Ijumaa dhidi ya Southampton ambapo Villa ilipokea kichapo cha 1-0 ugenini.

Mkurugenzi mtendaji wa Villa Christian Purslow amesema uamuzi huo uliafikiwa sasa ili kupatia kocha mpya atakayeteuliwa wakati tosha wa kufanya mabadiliko ya kuboresha klabu.

"Licha ya kuanza vizuri msimu uliopita, mwaka huu hatujaona uboreshaji endelevu wa matokeo, mwenendo na msimamo wa ligi ambao sote tumekuwa tukiutafuta. Kwa sababu hii tumeamua kufanya mabadiliko sasa ili kutoa muda kwa kocha mkuu mpya kufanya matokeo" Purslow alisema.

Villa imetangaza kwamba tayari wameanza juhudi za kusaka kocha atakayejaza nafasi iliyoachwa wazi na Smith.